You Are Here: Home » Whats New » TIMU YA YANGA YATANGAZA UTALII WA TANZANIA NI ULE WA “VISIT KILIMANJARO & ZANZIBAR”

TIMU YA YANGA YATANGAZA UTALII WA TANZANIA NI ULE WA “VISIT KILIMANJARO & ZANZIBAR”

SERIKALI kupitia kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, mapema leo Septemba 17,2021 imeingia makubaliano ya kutangaza Utalii wa Tanzania kupitia Mlima maarufu Duniani, Mlima Kilimanjaro pamoja na Visiwa vya Zanzibar kwa kuweka nembo katika jezi za timu ya soka ya Yanga kuelekea michezo ya Kimataifa ambapo imefanya hivyo pasipo malipo.

Akizungumza katika tukio hilo,  Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro ameipongeza timu ya Yanga kwa kuleta wazo hilo la kuutangaza Utalii wa Taifa, kupitia safari zake za Kimataifa katika mchezo wake wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United FC ya nchini Nigeria na michezo mingine kama itafanikiwa kufuzu raundi inayofuata.

“Timu ya Yanga wameweka nembo ya Mlima Kilimanjaro, visiwa vya Zanzibar katika Jezi zao zote, ili kutangaza utalii wa Tanzania bure kabisa bila hata malipo

Lakini kama wangetaka pesa basi ingekuwa zaidi ya Bilioni1 za Kitanzania kuweka nembo hii kwenye jezi hizo” amesema Dkt. Ndumbaro.

Hatua hiyo inakwenda sambamba na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kutangaza utalii wa nchi kupitia kipindi maarufu cha Royal Tour alichokianzisha yeye mwenyewe.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa Timu ya Yanga,  Haji Mfikirwa amesema Yanga inafanya hayo yote kuunga mkono jitihada za Tanzania kuendelea kutangaza utalii wake, na kwamba hiyo ni kutokana na kuwa na idadi kubwa ya mashabiki ndani na nje ya nchi kitendo kinachoweza kuvutia idadi kubwa ya Watalii duniani.

© 2021 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top