You Are Here: Home » Whats New » TAMKO LA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KUHUSU KUONGEZEKA KWA VITENDO VYA WANANCHI KUVAMIA, KUJERUHI

TAMKO LA WIZARA YA MALIASILI NA UTALII KUHUSU KUONGEZEKA KWA VITENDO VYA WANANCHI KUVAMIA, KUJERUHI

Wizara ya Maliasili na Utalii imepewa dhamana ya kusimamia Uhifadhi wa Maliasili, Malikale na Maendeleo ya Utalii. Katika kutekeleza majukumu hayo, Wizara inasimamia maeneo yaliyohifadhiwa kisheria yenye ukubwa wa kilometa za mraba takriban 307,800 sawa na asilimia 32.5 ya eneo lote la nchi.

Maeneo hayo yanajumuisha hifadhi za Taifa 22, Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, mapori ya akiba 22, mapori tengefu 27, maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi za wanyamapori 38, maeneo matatu (3) ya ardhi oevu chini ya Mkataba wa Ramsar, hifadhi za misitu ya asili 465, Hifadhi za Misitu ya Mazingira asilia 20, Mashamba ya Miti ya Serikali 24, hifadhi za nyuki 12, maeneo ya malikale 133 na vituo saba (7) vya Makumbusho ya Taifa.

Hivi karibuni kumekuwa na matukio mbalimbali ya wananchi wanaoishi karibu na maeneo yaliyohifadhiwa kuwavamia kwa silaha za jadi na za kivita askari wetu wa Jeshi la Uhifadhi Wanyamapori na Misitu (JU), wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao kisheria. Aidha, matukio haya yamekuwa yakijrudia mara kwa mara katika maeneo mbali mbali hapa nchini na mara nyingi yamekuwa yakitokea pindi askari wa Jeshi la Uhifadhi wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao ya ulinzi kama vile; kukamata mifugo na majangili wanaokutwa ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa kinyume cha Sheria.

Hata hivyo,  mifugo au baadhi ya wananchi wanapokamatwa kwa makosa ya kuingia ndani ya hifadhi kinyume cha sheria kumekuwa na tabia ya wananchi kujipanga na kuvamia askari au kambi zao na kuwashambulia kwa silaha mbalimbali za jadi kama vile fimbo, sime, mapanga, mishale n.k. Matukio hayo husambabisha baadhi ya askari wa Jeshi la Uhifadhi kujeruhiwa au kuuwawa pamoja na kusababisha uharibibifu wa mali za Serikali kama vile kuchoma moto magari, nyumba na vitendea kazi vingine muhimu kwa ajili ya shughuli za uhifadhi.

Katika kipindi cha hivi karibuni vitendo vya wananchi kujichukulia sheria mkononi dhidi ya askari wa Jeshi la Uhifadhi vimeongezeka. Aidha, idadi ya askari wanaouwawa na kujeruhiwa na wananchi hao imeongezeka. Taarifa tulizonazo zinaonesha kuwa hivi karibuni yametokea matukio zaidi ya manne ya askari wa Jeshi la Uhifadhi kuuwawa na kujeruhiwa na wananchi kama ifuatavyo;-

i. Tarehe 07 Machi, 2022, ndani ya Pori la Akiba Igombe lililopo mkoa wa Tabora, askari wa Jeshi la Uhifadhi walivamiwa na kushambuliwa na wananchi kwa kutumia silaha aina ya gobore. Katika shambulio hilo wananchi hao walimjeruhi askari wetu mmoja (1) kwenye bega la kushoto kwa risasi na kuharibu gari.

ii. Tarehe 06 Mei, 2022, ndani ya Pori la Akiba Igombe lililopo mkoa wa Tabora, askari wa Uhifadhi 11 na mgambo 32 walivamiwa na kushambuliwa na wananchi kwa kutumia silaha aina ya gobore. Tukio hilo lilipelekea kuuwawa kwa askari wawili wa Jeshi la akiba (Mgambo).

iii. Tarehe 09 Juni, 2022, ndani ya Pori Tengefu la Pololeti zamani Loliondo wananchi takiribani 200 wakiwa na silaha za jadi walivamia kambi ya askari na kumchoma mkuki askari polisi mmoja na kumsababishia kifo.

iv. Tarehe 31 Agosti, 2022 ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Makere Kusini wilayani Kasulu Mkoa wa Kigoma wananchi waliwavamia askari wa Jeshi la Uhifadhi na kufanya mauaji kwa kuwachinja askari wawili wa Suma JKT. Aidha, katika tukio hilo wananchi   hao pia walifanya uharibifu mkubwa wa mali kwa kuchoma kambi ya askari, pikipiki 6,  trekta 1 na mazao (gunia 70 za mahindi, 30 za mihogo, 20 za mtama na 20 za maharage) mali ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

v. Tarehe 8 Septemba, 2022 ndani ya Hifadhi ya Makere Kusini lililopo Mkoa wa Kigoma wananchi walivamia kambi ya askari wa Jeshi la Uhifadhi na kuchoma moto mahema, trekta na kunyunyizia sumu ya kuua miche kwenye vitalu.

vi. Tarehe 11 Septemba, 2022 ndani ya Hifadhi ya Makere Kusini, wananchi walivamia kambi ya askari na kuchoma sehemu ya shamba la miti ambapo Hekta 119 ziliungua kwa moto.

vii. Tarehe 17 Novemba, 2022, ndani ya Pori Tengefu la Kilombero, askari wa Jeshi la Uhifadhi walivamiwa na kundi la wafugaji waliokadiriwa kuwa kati ya 50 na 60 wakiwa na silaha za jadi (Fimbo, Sime na mapanga) kwa malengo ya kupora ng’ombe waliokuwa wamekamatwa ndani ya hifadhi. Katika tukio hilo askari wawili wa Jeshi la Uhifadhi walijeruhiwa vibaya kichwani na miguuni.

viii. Tarehe 20 Disemba, 2022 majira ya saa 8 usiku, kundi la wafugaji wanaokadriwa kuwa zaidi ya mia moja (100) wakiwa na silaha za jadi walivamia kambi ya askari wa Jeshi la Uhifadhi iliyopo katika Hifadhi ya Misitu ya Nyahua-wilayani sikonge kwa lenngo la kupora mifugo yao iliyokuwa imeshikwa Hifadhini. Katika tukio hilo askari 18 walijeruhiwa vibaya na kulazwa katika hosipitali ya rufaa ya Mkoa wa Tabora (kitete), magari 2 ya TFS kuchomwa moto, ng’ombe 1345 kuporwana kuibiwa kwa mali binafsi za askari.

ix. Tarehe 21 Januari 2023 ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, wananchi wa Kijiji cha Nyahungu Wilayani Tarime Mkoani Mara, walivamia askari wakiwa na silaha za jadi na kumchoma askari mshale wenye sumu kichwani na kumsababishia kifo.

x. Tarehe 31/01/2023 kikosi cha doria cha Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Kigoma ambacho kilikua na jumla ya watu 22,  kikiwa kwenye doria katika Hifadhi ya Msitu wa Kijiji cha Chakulu kikiongozwa na Afisa Misitu wa Wilaya (DFO) kilivamiwa na wafugaji kwa lengo la kupora mifugo yao iliyokuwa imekamatwa Hifadhini. Katika tukio hilo watu watatu (3) ambao ni Ndugu Adam Halenga (Afisa Misitu wa Wilaya), Ndugu Ibrahimu Seba (Mgambo) na Ndugu Shaban Kidonya wameuwawa na wengine wanne (04) walijeruhiwa vibaya na kukimbizwa hospitali.

Kufuatia hali hii, Wizara ya Maliasili na Utalii inalaani vikali vitendo hivi vya kihalifu vilivyofanywa na baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi na kusababisha vifo, majeruhi pamoja na uharibifu wa mali za serikali.

Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori ya Mwaka 2009, pamoja na sheria nyingine zizosimamia maeneo yaliyohifadhiwa zimekataza masuala mbalimbali kufanyika ndani ya maeneo ya hifadhi ikiwa ni pamoja na kukataza wananchi kuingia ndani ya maeneo hayo bila vibali, kufanyika kwa shughuli mbalimbali za kijamii kama vile kilimo, kulisha mifugo, uwindaji haramu wa wanyamapori na uvunaji haramu wa mazao ya misitu.

Wizara ya Maliasili na Utalii inawasisitiza wananchi waendelee kuwa mstari wa mbele katika kulinda rasilimali za Wanyamapori na Misitu hapa nchini na inawataka wale wote wanaojichukulia sheria mkononi kwa kuvamia maeneo yaliyohifadhiwa, kujeruhi au kuuwa askari wetu wa uhifadhi waache vitendo hivyo kwa kuwa ni kinyume cha Sheria za nchi. Aidha, Wizara kupitia Jeshi la Uhifadhi inaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama ili kukomesha vitendo hivi pamoja na kuwabaini wale wote wanaohusika kwa namna moja au nyingine ili Sheria ichukue mkondo wake.

  Imetolewa na:
……………………………
      Mhe. Balozi Dkt. Pindi H. Chana (Mb.)
                    WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII
                              Februari, 2023

 

© 2023 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top