You Are Here: Home » Whats New » SERIKALI YA TANZANIA IMESEMA WANANCHI WALIOHAMA KWA HIARI KUTOKA HIFADHI YA NGORONGORO KWENDA MSOMER

SERIKALI YA TANZANIA IMESEMA WANANCHI WALIOHAMA KWA HIARI KUTOKA HIFADHI YA NGORONGORO KWENDA MSOMER

Serikali ya Tanzania imeiambia Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu kuwa zoezi la kuwahamisha wananchi waliojiandikisha kwa hiari kutoka Hifadhi ya Ngorongoro kwenda katika Kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoa wa Tanga na maeneo mengine ni kulinda haki za Binadamu.

Kauli hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki Jijini Dodoma na baadhi ya Mawaziri wakati kikao kilichowakutanisha Mawaziri wa Tanzania pamoja na Timu ya Wataalamu kutoka Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu ikiongozwa na Kamishna wa Kamisheni hiyo, Dkt.Litha Ogana waliokuja nchini kufuatilia suala la kuhama wananchi wa Ngorongoro ambapo kabla ya kufanyika kwa mazungumzo hayo kamisheni hiyo ilipata fursa ya kutembelea na kufanya mazungumzo na wananchi Ngorongoro na Msomera.

Hatua ya Timu ya Wataalamu ya Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu kutua hapa nchini inakuja kufuatia malalamiko ya baadhi ya Asasi za Kiraia kuwa zoezi la kuwahamisha wananchi kwa hiari kutoka Ngorongoro kwenda katika Kijiji cha Msomera ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt.Pindi Chana ameieleza Kamisheni hiyo kuwa zoezi la kuwahamisha wananchi kwenda Msomera limefuata haki za binadamu kwa kwa lilikuwa shirikishi huku akibainisha kuwa bado wananchi wanaendelea kujiandikisha kwa hiari bila kushurutishwa kwa kuzingatia ipasavyo utu, heshima na haki za binadamu.

Amefafanua kuwa Serikali iliamua kufanya maamuzi hayo kwa kuwa Wananchi wa Ngorongoro walikuwa hawawezi kumiliki ardhi, kujenga makazi bora na ya kudumu na kufanya mambo yao ya maendeleo kwa ajili ya mustakabali wa familia zao kwa kuwa yalikua yanayokinzana na Sheria ya Uhifadhi

Mbali na hilo, Dkt.Pindi Chana ameieleza Timu hiyo kuwa wananchi wanaoishi Ngorongoro wamekuwa wakikumbana na kadhia nyingi ambapo katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020 takribani wananchi 50 waliuawa na Wanyamapori wakali na waharibifu huku wananchi 148 walijeruhiwa na wanyamapori hao na kuwasababishia vilema vya kudumu

Ameelezea kuwa wananchi waliohamia kijiji cha Msomera wamelipwa fidia, wamejengewa nyumba zenye staha pamoja na kupewa hati ya kumiliki ya ardhi pamoja na kupatiwa huduma zote za kijamii ambazo walipokuwa Ngorongoro walizikosa


” Serikali imeendelea kuwapa stahiki zao wananchi wote wanaohama kwa hiari ikiwa ni pamoja na kuwapa fidia inayostahili pamoja na kuwasafirishia mizigo,  mali na mifugo yao kuelekea kwenye makazi mapya na huu ndo msingi wa haki za binadamu ” amesisitiza Mhe.Balozi Dkt.Pindi chana

Ameongeza kuwa ” Wananchi wa Ngorongoro hususan watoto kwa kipindi kirefu walikosa haki ya kupata elimu bora, haki ya kuishi bila woga na haki ya kucheza kutokana na hofu ya kushambuliwa na wanyamapori wakali na waharibifu hivyo kitendo cha kuhamia Msomera watoto hao watapata haki zao za msingi kama ilivyo kwa watoto wa maeneo mengine ” amesisitiza Balozi Dkt.Chana

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kikao hicho ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt.Damas Ndumbaro alisema kwa sheria zilizopo Tanzania hakuna kabila lolote linalomiliki ardhi ya mababu zao hivyo madai ya kwamba Maasai wanatolewa kwenye ardhi ya mababu zao halina msingi wowote.

Amesema tangu kuanza kwa zoezi la kuwahamisha kwa hiari wananchi hao haki zao kama binadamu zimezingatiwa kwa kiasi kikubwa huku utu, heshima na staha vikipewa kipaumbele na serikali.

Naye Kamishna wa Kamisheni ya Afrika ya Haki za Binadamu, Dkt.Litha Ogana amesema Kamisheni hiyo imejiridhisha kuwa haki imetendeka katika kuwahamisha wakazi wa Ngorongoro na hakukuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu

” Tumejionea wenyewe tumeona haki zao, tamaduni zao na mchakato mzima wa kuwahamisha ulikuwa ni shirikishi, amesema Dkt.Litha Ogana

Itakumbukwa kuwa zoezi la kuhamisha wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro waliojiandikisha kuhama kwa hiari kwenda Kijiji cha Msomera lililoanza mwezi Juni, 2022, hadi kufikia Januari, 2023 Jumla ya kaya 523 zenye watu 2,808 na mifugo 14,757 zimeshahamia Kijiji cha Msomera na maeneo mengine kwa ajili ya kulinda haki za binadamu.

 

 

© 2023 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top