You Are Here: Home » Whats New » ONESHO LA KWANZA LA UTALII LA EAC 2021 KUFANYIKA TANZANIA

ONESHO LA KWANZA LA UTALII LA EAC 2021 KUFANYIKA TANZANIA

Ndugu Wanahabari;

Awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa leo. Aidha, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwenu kwa kuitikia wito huu. Ni dhahiri kuwa vyombo vya habari mmekuwa mabalozi wetu wazuri katika kufanikisha shughuli mbalimbali za uhifadhi na uendelezaji wa utalii nchini.

Ndugu Wanahabari;
Katika jitihada za kuvutia watalii na kukuza uwekezaji katika sekta ya utalii, mwezi Julai 2021 Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wanaoshughulikia masuala ya wanyamapori na utalii walipitisha Mkakati wa Kutangaza Utalii wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (East African Community Marketing Strategy, 2021 – 2025). Miongoni mwa masuala yaliyomo katika Mkakati huo ni kuanzishwa kwa Onesho la Utalii la Jumuiya ya Afrika Mashariki (East African Regional Tourism Expo – EARTE). Onesho hili litakuwa linafanyika kwa mzunguko katika nchi wanachama kila mwaka.

Ndugu Wanahabari;
Napenda kuwajulisha kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndio itakuwa Mwenyeji wa kwanza wa Onesho hili   la Utalii la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kauli mbiu ya Onesho hilo ni “Utangazaji Utalii Stahimilivu kwa Maendeleo Jumuishi ya Kijamii na Kiuchumi” (Promotion of Resilient Tourism for Inclusive Socio-Economic Development). Onesho la EARTE litafanyika Jijini Arusha kuanzia tarehe 9 hadi 16 Oktoba, 2021 ambapo litajumuisha siku tatu (3) za maonesho (exhibition), na siku tano (5) za ziara maalum kutembelea vivutio vya utalii (FAM trips) pamoja na fursa za utalii wa ndani kwa Tanzania Bara na Zanzibar.

Ndugu Wanahabari;
Kutakuwa na matukio mbalimbali ikiwemo jukwaa la uwekezaji na semina zitakazohusisha mada tofauti kama vile; Utalii Stahimilivu na Hatua za kukabiliana na Majanga; Utangazaji Utalii Kimtandao; Utangazaji wa Vifurushi vinavyojumuisha Vituo vya Utalii tofauti; Ushirikiano wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kukabiliana na Ujangili na Biashara Haramu ya Wanyamapori; na Fursa za Kiuchumi za Sekta ya Wanyamapori. Mada hizo zitawasilishwa na Wataalamu kutoka ndani na nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Pia, Onesho hilo litahusisha waoneshaji (exhibitors), wanunuzi wa kimataifa (international buyers), wawekezaji, na wageni kutoka nchi mbalimbali.

Ndugu Wanahabari;
Kwa kutambua utalii ni sekta mtambuka, Onesho hili ni fursa muhimu ya kuhamasisha uhifadhi wa maliasili na malikale pamoja na kuchochea ukuaji wa utalii hususan utalii wa mikutano na matukio (MICE Tourism) ambao ni zao jipya la utalii la kimkakati la kufanikisha lengo la kuongeza idadi ya watalii katika ukanda wa Afrika Mashariki. Vilevile, litasaidia kuimarisha ushirikiano baina ya nchi wanachama.


Ndugu Wanahabari;
Kupitia kwenu naomba kutoa rai kwa ndugu zangu watanzania hususan wakazi wa Jiji la Arusha, watoa huduma za malazi, wakala wa biashara za utalii, wakala wa safari na waongoza watalii kuchangamkia fursa za kiuchumi na kijamii zitakazotokana na onesho hili. Aidha, nawaomba wanahabari mshiriki kikamilifu katika kutangaza onesho hili ili kuvutia ushiriki wa wadau wengi katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

Kwa taarifa zaidi kuhusu onesho la EARTE unaweza kutembelea tovuti ya onesho hilo ambayo ni https://eacexpo.tanzaniatourism.go.tz.


ASANTENI KWA KUNISIKILIZA

PRESS_RELEASE_YA_NAIBU_WAZIRI_EARTRE-1_OG_yamwisho

© 2021 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top