You Are Here: Home » Whats New » NAIBU KATIBU MKUU JUMA S. MKOMI AKAGUA UTEKELEZAJI MIRADI YA UVIKO 19 - KITUO CHA MAKUMBUSH

NAIBU KATIBU MKUU JUMA S. MKOMI AKAGUA UTEKELEZAJI MIRADI YA UVIKO 19 - KITUO CHA MAKUMBUSH

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Juma S. Mkomi amefanya ziara ya kikazi ya kukagua matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali kugharamia miradi mbalimbali katika kituo cha Makumbusho ya Elimu Viumbe kilichopo Jijini Arusha.

Fedha hizo ni zile za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19, ambapo Makumbusho ya Taifa la Tanzania ilipatiwa kiasi cha shilingi Bilioni 2.4 ili iweze kutekeleza miradi 15 katika vituo mbalimbali kikiwemo kituo cha Makumbusho ya Elimu Viumbe Arusha.

Naibu Katibu Mkuu, Juma Mkomi akiwa kwenye ziara hiyo amepokea taarifa ya kazi mbalimbali zilizofanyika kupitia fedha za UVIKO 19, iliyotolewa na Mkurugenzi wa Makumbusho hiyo, Dkt. Christina Ngereza na kukagua mradi wa onesho la tembo na ujenzi wa taswira za wanyamapori watano wakubwa wanaovutia utalii wa wanyamapori, maabara ya Biolojia, onesho la Reptilia, na uboreshaji wa stoo ya uhifadhi wa mikusanyo ya bailojia.

Pia amekagua kazi mbalimbali zilizofanyika kupitia fedha hizo zikiwemo ujenzi wa vyoo vipya, uwekaji wa taswira za wanyamapori wakubwa wanaopatikana nchini Tanzania ambao wamekua kivutio kikubwa kwa watalii na kukagua mifumo ya Kamera ya Usalama (CCTV Camera) iliyowekwa, samani mbalimbali na kazi ya uimarishaji wa mifumo ya TEHAMA iliyofanyika.

Aidha, amepata fursa ya kutembelea ofisi ya wataalam wanaojenga taswira mbalimbali za wanyamapori hapa nchini ambayo ipo katika kituo hicho na kutembelea eneo lenye Kobe aliyehifadhiwa anayekadiriwa kuwepo kabla ya Uhuru wa Tanganyika ambaye aliletwa nchini kama zawadi kwa Mfalme aliyekuwepo wakati huo.

Katika ziara hiyo ya kukagua miradhi ya UVIKO 19, Naibu Katibu Mkuu Juma Mkomi ameambatana na Dkt. Consolatha Kapinga, Mchumi Mwandamizi na Mratibu wa Miradi ya UVIKO -19 kutoka Idara ya Sera na Mipango ya Wizara ya Maliasili na Utalii.

© 2023 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top