You Are Here: Home » Whats New » MATOKEO YA SENSA YA WANYAMAPORI KWA MWAKA 2022

MATOKEO YA SENSA YA WANYAMAPORI KWA MWAKA 2022

Wizara ya Maliasili na Utalii inapenda kuujulisha umma matokeo ya sensa ya wanyamapori iliyofanyika kuanzia tarehe 21 Septemba hadi tarehe 10 Oktoba 2021 kwenye mfumo Ikolojia wa Katavi – Rukwa na Ruaha-Rungwa yenye eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 88,718.

Sensa hizi hufanyika kila baada ya miaka mitatu kwa lengo la kujua uwepo, Idadi, mtawanyiko na viashiria hatarishi kwa ustawi wa wanyamapori. Zoezi hili liliwezeshwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Asasi ya Kiraia ya Jumuiya ya Uhifadhi Wanyamapori (Wildlife Conservation Society - WCS) na kuratibiwa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI).
Wizara inaujulisha umma idadi ya wanyamapori kwa kila mfumo ikolojia na taarifa kamili ipo tayari kwa rejea na itapatikana wizarani na TAWIRI.
Matokeo ya sensa katika mifumo ikolojia ya Katavi - Rukwa na Ruaha -Rungwa ni kama ifuatavyo :

a) Mfumo ikolojia wa Katavi–Rukwa
Katika eneo hili, sensa ilibaini uwepo wa aina 22 za wanyamapori. Aidha, kati ya aina hizo za wanyamapori zilizoonekana kwa wingi ni nyati 35,273, kongoni 9,027, pundamilia 5,223, tembo wapatao 4,132, pofu 3,947 na ngiri 3,922. Aina za wanyamapori walioonekana kwa uchache zaidi ni pamoja na tandala wakubwa waliokadiriwa kuwa 526 na pongo wapatao 400.
Tanzania inaongoza kwa idadi ya nyati Barani Afrika wengi wao wakiwa katika mifumo ikolojia ya Serengeti (69,075), Nyerere-Selous-Mikumi (66,546), Katavi-Rukwa (35,273) na Ruaha-Rungwa (20,911).
Idadi ya tembo imeendelea kuimarika na viashiria vya ujangili wa tembo au vifo vimeendelea kupungua ukilinganisha na sensa ya mwaka 2018. Mwaka 2021, uwiano wa mizoga mipya ilikuwa asilimia 3 wakati mwaka 2018 ilikuwa asilimia 12.
Idadi ya wanyamapori wengine imendelea kuimarika kwa mfano korongo wameendelea kuongezeka na idadi yao kwa sasa ni 2,501 ukilinganisha na korongo 2061 waliohesabiwa mwaka 2018. Ongezeko hili ni asilimia 20 kati ya miaka husika. Mfumo ikolojia wa Ruaha-Rungwa na Katavi Rukwa ndio sehemu muhimu kwa uhifadhi wa korongo nchini.
Aidha, matokeo yameonyesha kuwa kwa sasa mfumo ikolojia wa Katavi-Rukwa una idadi ya sheshe (puku) isiyozidi 700, ukilinganisha na sheshe takribani 3,000 waliohesabiwa kwenye sensa ya mwaka 2018. Kwa ujumla, wanyamapori aina sheshe wameendelea kupungua hivyo jitihada maalum zinahitajika kuhakikisha wanyamapori hawa wanaendelea kustawi na kuwepo Tanzania.

Viashiria hatarishi kwa ustawi wa wanyamapori
Pamoja na kuhesabu wanyamapori katika mfumo huu, zoezi hili pia lilifanya utambuzi wa viashiria hatarishi katika uhifadhi. Matokeo yamebainisha kwamba shughuli za kibinadamu, zikiwemo ufugaji, makazi na kilimo mkabala au ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa zimeendelea kuwa changamoto kwenye mfumo ikolojia huu.  Kwa sensa ya mwaka 2021 idadi ya ng’ombe walioonekana ndani ndani ya mfumo huuilikuwa 70,000. Shughuli nyingine za kibinadamu ni pamoja na makazi ya binadamu nyumba za nyasi 7,700, matukio ya uvunaji wa mbao 3,000, na ufugaji wa nyuki ambapo jumla ya mizinga ya nyuki 4,700 ilihesabiwa. Hali hii, inaonyesha wazi kuwa shughuli za kibinaadamu zinaendelea kuwa tishio kubwa kwa uhifadhi endelevu wa mfumo ikolojia wa Katavi Rukwa hivyo wizara inaendelea kuchukua hatua madhubuti kuleta usawa wa maisha ya binadamu, wanyamapori na mazingira kwa ujumla.

(b) Mfumo ikolojia wa Ruaha–Rungwa
Matokeo ya sensa kwenye mfumo Ikolojia huu ulibaini aina za wanyamapori 24. Aina za wanyamapori zilizoonekana kwa wingi ni pamoja na nyati ambao kwa wastani walikuwa 20, 911, tembo 15,751, pundamilia 10,550, swala pala 8,643, na palahala 6,996.
Kwa ujumla idadi ya tembo imeendelea kuimarika kwenye mfumo Ikolojia huu ambao ulikuwa miongoni mwa maeneo yalioathiriwa zaidi na matukio ya ujangili katika miaka ya 2013/14. Uwiano wa mizoga mipya na idadi ya tembo katika sensa hii imepungua kwa kiasi kikubwa, ikiwa ni asilimia 1.4 ikilinganishwa na asilimia 14 ya mwaka 2018. Hii inatokana na jitihada kubwa za kimkakati za serikali na wadau wa uhifadhi katika kuimarisha ulinzi wa wanyamapori.
Aidha, idadi ya wanyamapori adimu kama korongo na palahala imeendelea kuongezeka. Korongo wameongezeka mara mbili toka korongo 1,436 mwaka 2018 hadi 3,127 kwa sensa ya mwaka 2021. Hawa ni mojawapo ya wanyamapori adimu wanaoendelea kupungua katika maeneo mengine mfano katika mfumo Ikolojia Serengeti ambako wanyamapori hao wamepungua zaidi na huonekana kwa nadra saana. Watalaam wanakisia idadi yao kuwa chini ya 20.
Kwa upande mwingine idadi ya nyati imeendelea kufanya vizuri hasa katika maeneo ya ndani ya hifadhi ongeeko likiwa ni ni asilimia 64% toka mwaka 2018. Pamoja na kuwepo kwa changamoto za mifugo katika mfumo Ikolojia huu ongezeko la nyati ni kiashiria kizuri cha udhibiti wa mifugo kwenye maeneo yaliohifadhiwa.

Viashiria hatarishi kwa ustawi wa wanyamapori
Katika kipindi cha miaka mitatu (2018-2021), uvamizi wa ng’ombe katika mfumo ikolojia huu umeongezeka kwa kiwango cha asilimia 82% na mbuzi/kondoo kwa asilimia 5%. Kwa kipindi cha sensa ng’ombe walikuwa 393,519 na mbuzi/kondoo 139,663 toka ng’ombe 216,663 na mbuzi/kondoo 133,331 mwaka 2018. Pia changamoto ya uvunaji haramu wa miti maeneo ya Rungwa na Kizigo imeendelea kuonekana ambapo jumla ya matukio 4,271 yalionekana wakati wa sensa sambamba na ongezeko la mashamba eneo la bonde la Usangu katika Hifadhi ya Taifa Ruaha. Changamoto hizi zimepelekea uharibifu mkubwa wa makazi na malisho ya wanyamapori pamoja na kusababisha kiasi cha maji kwenye bonde la mto Ruaha Mkuu kupungua.

Vitisho vinavyoathiri mifumo ikolojia ya Katavi–Rukwa na Ruaha-Rungwa
i. Ongezeko kubwa la uvamizi wa mifugo, ukataji haramu wa misitu, kilimo, makazi na shughuli nyingine za kibinadamu, ndani ya maeneo yaliyohifadhiwa ni tishio kubwa kwa ustawi wa wanyamapori. Hali hii inaweza kusababisha kutoweka kwa baadhi ya aina za wanyamapori kutokana na kupungua kwa malisho au kutoweka kwa makazi yao.

ii. Ongezeko la mwingiliano kati ya binadamu, mifugo na wanyamapori kutaongeza uwezekano wa maambukizi ya magonjwa (zoonotic diseases). Hali hii pia inachangia kuongezeka kwa migogoro kati ya wanadamu na wanyamapori katika mifumo hii ya kiikolojia.

Mwisho
Kwa ujumla takwimu za sensa hii zimeonyesha kuna mwingiliano mkubwa kati ya binadamu, mifugo na wanyamapori. Eneo la bonde la usangu katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha shughuli za kibinadamu kama kilimo na mifugo zimeonekana kwa kiasi kikubwa hivyo serikali inaendelea na hatua za kuwaondoa wavamizi kwenye maeneo haya
Aidha tafiti zinaonesha mwingiliano wa aina hii unaongeza uwezekano wa kuongezeka kwa maambukizi ya magonjwa (zoonotic diseases) na migogoro kwenye maeneo yaliohifadhiwa.
Kwa muktadha huo,  ninazielekeza Mamlaka za Usimamizi wa Wanyamapori na Misitu kuimarisha ulinzi wa mipaka ya hifadhi dhidi ya ongezeko la shughuli za kibinadamu.
Aidha wizara itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo na uhifadhi kuwezesha uandaaji mipango ya matumizi bora ya ardhi na kuzishauri mamlaka zinazosimamia vijiji kuendelea kusimamia mipango ya matumizi bora ya ardhi ili kupunguza migongano kati wanyamapori na wananchi.
Sambamba na hilo nawaelekeza TAWA ambao ndio wenye maeneo yaliobaki na Sheshe (puku) washirikiane na TAWIRI kuhakikisha wanyamapori hawa hawatoweki katika mfumo ikolojia wa Katavi-Rukwa, hii ni pamoja na kuaandaa mkakati wa kuhakikisha wanyama hao wanaendelea kushamiri.
Mwisho kabisa nichukue fursa hii kutoa shukurani za dhati kwa Wildlife Conservation Society (WCS) kwa ushirikiano waliouonesha kufanikisha sensa hii.


Imetolewa na
Waziri wa Maliasili na Utalii
01/11/2022

© 2023 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top