You Are Here: Home » About Us » WAZIRI DKT. NDUMBARO AAHIDI KUKUTANA NA WADAU WANAOMILIKI VITALU VYA UWINDAJI

WAZIRI DKT. NDUMBARO AAHIDI KUKUTANA NA WADAU WANAOMILIKI VITALU VYA UWINDAJI

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro ametoa ahadi ya kukutana na Wadau wa Uwindaji wa Kitalii wanaomiliki Vitalu vya Uwindaji nchini Tanzania ambao sio wanachama wa Chama cha Uwindaji wa Kitalii Tanzania (TAHOA), Mwanzoni mwa mwezi Februari mwaka huu.

Kauli hiyo ameitoa leo Jijini hapa Las Vegas Nevada, Marekani wakati akitoa wito kwa Kamati ya watu 10 aliyoiounda kwa ajili ya kumshauri yeye kama Waziri namna bora ya kuendesha sekta ya uwindaji ya kitalii kuwasilisha ripoti itakayomsaidia kuboresha minada ya kielektroniki ya Biashara ya uwindaji wa Kitalii inayofuata hapo baadae.

Dkt. Ndumbaro amesema kuwa, mkutano huo utakuwa na lengo la kuboresha mazingira ya biashara ya sekta hiyo ikiwemo uzoefu walioupata katika ushiriki wa Maonesho ya 50 ya mwaka ya Uwindaji wa Kitalii yanayoendelea yakiwakutanisha watunga sera na wafanya maamuzi kutoka nchi mbalimbali Duniani juu ya kuendeleza sekta ya uwindaji.

Akizungumzia juu ya Kamati aliyoiunda Juni 23, 2021 Jijini Dodoma ya watu 10 ikiwa na watu watano kutoka Sekta binafsi na wengine watano kutoka Serikalini kushindwa kuwasilisha ripoti ya ushauri huo hadi leo.

Dkt. Ndumbaro amewataka Wadau hao wanaomiliki vitalu vya uwindaji vya kitalii nchini Tanzania kuacha kulalamika baadala yake wawasilishe ripoti hiyo ya ushauri kwa kuonesha yale waliyokubaliana kwa pamoja na yale waliyotofautiana ili yeye kuifanyia kazi ripoti hiyo

Amesema kitendo cha Kamati hiyo kushindwa kuiwasilisha ripoti hiyo kwa wakati kumempelekea yeye kama Waziri katika wakati mgumu katika kufanya maamuzi yenye maslahi mapana pande zote mbili yaani kwa Serikali na Wadau wa Sekta hiyo.

Amesema kuwasilishwa kwa ripoti hiyo mapema kutatoa muelekeo wa namna bora ya kuendesha minada ya kielektoniki ya Uwindaji wa Kitalii inayofuata katika mazingira bora zaidi.

“Baadhi yenu mmekuwa mkilalamika tu kuwa hamtaki minada wa kielektoniki wa vitalu vya uwindaji wa Kitalii, leteni ushauri kupitia ripoti hiyo mkionesha sababu na njia mbadala kama Serikali nini tufanye” alisema Dkt. Ndumbaro.

Kufuatia hali hiyo, Dkt.Ndumbaro amewasisitiza Wadau hao waliopo nchini Marekani ambao ni Washiriki wa Maonesho hayo 50, kuiwasilisha ripoti hiyo mapema iwezekanavyo ili mwanzoni mwezi Februari aweze kuitisha mkutano wa Wadau hao.

Hata hivyo, Dkt. Ndumbaro amewapongeza Wadau hao kwa maoni mazuri waliyoyatoa katika kikao alichofanya nao nchini hapa huku akiwasisitizia kuuweka ushauri huo katika maandishi na kuwasilisha ofisini kwake kwa lengo kuiwezesha Serikali na wadau hao kunufaika kupitia Biashara hiyo.

Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Uwindaji wa Kitalii (TAHOA), Michel Matheakis alimshukuru Waziri kwa kuwa muumini wa mazungumzo na kuahidi kuwa ripoti hiyo itawasilisha kwa ajili ya kufanyiwa kazi.

© 2024 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top