You Are Here: Home » Whats New » Serikali Kuanzisha Mfumo Mpya Wa Kuwalinda Wanyamapori

Serikali Kuanzisha Mfumo Mpya Wa Kuwalinda Wanyamapori

Serikali Kuanzisha Mfumo Mpya Wa Kuwalinda Wanyamapori

Wadau wa uhifadhi wa kitaifa na kimataifa wamekutana jijini Dar es Salaam na kujadili jinsi ya kuwezesha mfumo mpya utakaowezasha kulinda wanyamapori.
Akifungua mkutano huo jijini hapa leo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete,Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, alisema anaamini mkutano huo utaleta mabadiriko katika vita inayoendelea dhidi ya ujangili nchini.

Alisema mkutano huo utasaidia kuokoa tembo walioko hatarini kutoweka kutokana na ongezeko kubwa la hitaji la meno ya tembo na bei nzuri ilioyopo katika masoko yasiyo rasmi ya kimataifa.
Dkt. Bilal alisema mtandao wa majangili ndani na nje ya nchi ni mkubwa na hivyo serikali pekee haiwezi kukomesha ujangili nchini, na hivyo imeamua kuishirikisha Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya kutoa vitendea kazi vitakavyosaidia kuhifadhi tembo.

“Serikali inafanya kila inaloweza kuhakikisha inakomesha ujangili nchini ikiwemo kufanya doria za mara kwa mara pamoja na kuendesha operesheni mbalimbali. Hata hivyo, inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa fedha, vitendea kazi, tekinolojia na mafunzo. Hivyo naomba wadau wa uhifadhi kutuunga mkono katika vita dhidi ya ujangili,” alisema Mhe. Dkt. Bilal.
Dkt. Bilal aliongeza kuwa, hatima ya wanyamapori na tembo nchini inategemea uwepo wa ulinzi imara utakaowahakikishia wanyamapori kuishi salama katika mazingira halisi.
Aliongeza kuwa katika kuhakikisha usalama wa wanyamapori nchini, serikali tayari imeanda mpango mkakati wa vita dhidi ya ujangili ambao utazinduliwa hivi karibuni.

Akizungumza juu ya mkutano huo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Lazaro Nyalandu alisema Tanzania ndiyo nchi muhimili wa uwepo wa tembo barani Afrika na hivyo Watanzania kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa wanajukumu la kuhakikisha wanawalinda tembo hao.

Mhe. Nyalandu alisema mkutano huo umelenga kuhakikisha Jumuiya ya Kimataifa inashirikiana kutoa vitendea kazi huku serikali ikitoa rasilimali zote zilizopo ikiwa ni pamoja na rasilimali watu na miundo mbinu wezeshi ya yakuhakikisha mfumo mpya utakaowezesha kuwalinda wanyamapori unaanzishwa.

© 2023 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top