You Are Here: Home » Whats New » WAZIRI MKUU MHE. KASSIM MAJALIWA AWAAGIZA WAKUU WA MIKOA KUJENGA NYUMBA ZA ASILI KIJIJI CHA MAKUMBUS

WAZIRI MKUU MHE. KASSIM MAJALIWA AWAAGIZA WAKUU WA MIKOA KUJENGA NYUMBA ZA ASILI KIJIJI CHA MAKUMBUS

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa wote nchini kuhakikisha wanajenga nyumba za asili ya Mikoa yao kwenye ramani ya Tanzania iliyoandaliwa katika kijiji cha Makumbusho jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo inakuja ikiwa ni uboreshaji wa mpangilio wa nyumba hizo katika kijiji hicho kwa kuzijenga kulingana na ramani halisi ya Tanzania badala ya zilivyo sasa.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utaliii, Mhe. Japhet Hasunga ametoa maagizo hayo kwa niaba Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa wakati akifunga tamasha la utamaduni wa mtanzania inayowakilishwa na jamii za mkoa wa Lindi lililofanyika kwa muda wa siku nne katika kijiji cha Makumbusho jijini Dar es salaam

Amesema kujengwa kwa nyumba hizo kwa mujibu wa ramani kutawasaidia watalii watakaokuwa wakitembelea kijijini hapo kwenda moja kwa moja kuangalia nyumba ya kabila fulani endapo kama watakuwa wamepanga kufanya hivyo.

Kufuatia agizo hilo, Waziri Mkuu Majaliwa ameitaka Taasisi ya Makumbusho ya Taifa ihakikishe inashirikiana na jamii za Mikoa ili iweze kutengeneza “Operational Manual” ya nyumba za asili zitakazojengwa katika kijiji hicho.

Katika hatua nyingine. Waziri Mkuu huyo ameuagiza Mkoa wa Lindi uanzishe Makumbusho ya Mkoa yatakayosaidia katika kuhifadhi pamoja na kuelimisha umma juu ya historia, utamaduni, maendeleo na uchumi wa mkoa huo.

Ameongeza kuwa kujengwa kwa Makumbusho kutasaidia kuongeza mapato kupitia watalii watakaokuwa wakija kwa ajili ya kutembelea katika Makumbusho hiyo

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa wa Lindi, Mhe Godfrey Zambi amesema mkoa wa Lindi umejaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii hivyo amewataka wawekezaji wachangamkie fursa ya kuwekeza katika mkoa huo ili kutimiza azma ya serikali ya tano ya kuendeleza utalii kusini.

.Amesema mbali ya utajiri wa utamaduni wa jamii za Mkoa wa Lindi ambao ni sehemu muhimu katika utamaduni wa mtanzania, Mkoa huo umejaliwa kuwa na fukwe nzuri ambazo o hazijaguswa.

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top