You Are Here: Home » Whats New » UTALII WA KIUTAMADUNI WAPIGIWA CHAPUO MKOANI KIGOMA

UTALII WA KIUTAMADUNI WAPIGIWA CHAPUO MKOANI KIGOMA

Katibu tawala wa mkoa wa Kigoma, Charles Pallangyo amewataka wadau wa utalii kuchangamkia fursa za utalii hasa utalii wa Kiutamaduni kwa kuwa ni utalii usio na gharama katika kuuanzisha

Amesema watalii wanaokuja nchini kwa sasa wanakuja kwa ajili ya kuijifunza tamaduni zetu kama vile jinsi jamii zetu zinavyoishi na zinavyokula vyakula vyao na si kuona wanyamapori pekee.

Akizungumza jana mjini Kigoma wakati akifungua warsha ya kukusanya maoni ya wadau kwa ajili mapitio ya Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 1999.  Palangyo alisema sera hiyo inaboreshwa ili iweze kuendana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea duniani ya kiteknolojia, kijamii, kiuchumi, kisiasa na mazingira.

Ukusanyaji maoni huo umeshirikisha wataalamu wa utalii, maofisa utalii, mahotelia, sekta binafsi pamoja na watu wanaojishughulisha na biashara ya utalii moja kwa moja kutoka katika mkoa wa Kigoma, Katavi na Rukwa.

Amesema mikoa ya Magharibi inaweza kujitofautisha na mikoa mingine kwa kuwa na utalii wa kipekee kwa vile ina vivutio vya utalii vya aina mbalimbali ukiachilia mbali Hifadhi ya Taifa ya Gombe, Mahale na Katavi.

Akitaja baadhi ya vivutio hivyo mbali na hifadhi hizo ni uwepo wa makabila mbalimbali, nyumba ya makumbusho ya Dkt. David Livingstone, Ziwa Tanganyika, maporomoko ya Kalambo, sehemu za matambiko pamoja na uwepo wa meli ya Mv Liemba.

Awali, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Martini Mrema amesema sera hiyo inapitiwa upya ili kuhakikisha kuwa utalii wa nje ya hifadhi unaanza kupewa kipaumbele tofauti na sasa.
 
Aliongeza kuwa sera hiyo inaboreshwa ili iweze kujibu changamoto za utalii wa sasa

Kwa upande wake Mdau wa utalii, Jonathan Lucas wa mkoa wa Katavi alichangia kuwa sera hiyo itamke wazi namna mtu mmoja mmoja atakavyonufaika na vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Mchakato huu wa kukusanya maoni ya wadau unafanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo Benki ya Duniani (WB) chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, wadau wa Sekta Binafsi pamoja na Shirikisho la Vyama vya Utalii Tanzania (TCT).

 

 

 

 

 

© 2018 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top