You Are Here: Home » Whats New » TAASISI ZA UHIFADHI   ZAAGIZWA KUTUMIA SPORT TOURISM KUNADI VIVUTIO VYA UTALII

TAASISI ZA UHIFADHI   ZAAGIZWA KUTUMIA SPORT TOURISM KUNADI VIVUTIO VYA UTALII

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu amezitaka Taasisi za uhifadhi na utalii nchini zianze kuitazama fursa ya utalii michezoni(Sport Tourism) kwa namna ya kipekee na kuiwekea mkakati wa namna ya kuitumia.

Pia amezitaka taasisi hizo zianze kudhamini wanamichezo pamoja na michezo mbalimbali ikiwemo Mpira wa miguu, mpira wa pete pamoja na mchezo wa ngumi kwa sababu imekuwa ikitumika sana kuitangaza nchi pamoja na vivutio vya utalii.

Ametoa maagizo hayo leo mara baada ya kumalizika mashindano ya Serengeti Safari Marathon yaliyofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa upande wa geti la Ndabaka mkoani Simiyu.

Mashindano hayo yaligawanyika kwa wakimbiaji wa mbio za kilomita 42, 21 pamoja mbio za kilomita tano.

Amesema utalii wa kimichezo ukitumika ipasavyo utakuwa na mchango mkubwa katika kuunga mkono dhamira ya Serikali ya kuongeza idadi ya watalii na mapato yatokanayo na utalii

Kwa upande wake Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Serengeti Safari Marathoni Henrick Kimambo amesema mchezo huo utasaidia kuhamasisha jamii pamoja na kuchochea jamii kuvihifadhi vivutio vya utalii vilivyopo nchini.


Aidha, Mkurugenzi huyo mesema wameamua kuanzisha michezo hiyo kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii kimataifa kwa kuwashirikisha wanamichezo kutoka ndani na nje ya nchi.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Hifadhi za Taifa (TANAPA), Paschal Shelutete ambao ni miongoni mwa wadhamini wa mashindano hayo, Amesema mashindano hayo ni muhimu katika kutangaza vivutio vya utalii nchini


Kwa upande wake Mwakilishi wa Rais wa chama cha riadha nchini, Yohana Misese amewaomba wananchi watumie fursa hiyo ya michezo katika kutangaza vivutio vya utalii.

Pia, Ameiomba serikali kuangalia namna ya kuwadhamini katika katika mchezo wa mbio ili kupunguza tatizo la ajira nchini na kuongeza kuwa wanashindwa kupeleka washiriki nchi za nje kutokana na ukosefu wa fedha.

Naye, Mpima njia katika mashindano hayo,  Filiberti Bayi amesema michezo hiyo ni fursa muhimu katika kukuza vipaji na wakati huo huo kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Hata hivyo katika mashindano hayo, Kenya ndio iliyoongoza kwa washindi wa mbio ndefu na fupi ndio kuibuka kidedea kwa kunyakua pesa taslimu ambapo mshindi wa kwanza amezadiwa shilingi milioni 2 pamoja na medali.

 

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top