You Are Here: Home » Whats New » SERIKALI YAUZA MENO YA VIBOKO KWA SH.30,900,000/= KATIKA MNADA

SERIKALI YAUZA MENO YA VIBOKO KWA SH.30,900,000/= KATIKA MNADA

Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imefanya mnada wa hadhara wa kuuza meno ya viboko vipande 12,467 yenye uzito wa kilo 3,580.29 katika ofisi ndogo ya Wizara ya Maliasili na Utalii katika Jengo la Mpingo, jijini Dar es Salaam


\Katika mnada huo jumla ya makampuni 19 yenye leseni daraja la kwanza yameshiriki .

Mnada huo umefanyika chini ya usimamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango ambapo kampuni ya On Tours Tanzania Limited imeibuka mshindi kwa kununua meno hayo kwa jumla ya shilingi 30,900,000/=

Awali akizungumza katika mnada huo, Mwenyekiti kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Karerema Kwaleh aliwataka wafanyabiashara hao kuzingatia masharti mnada huo.

Ambapo Karerema alimtaka mfanyabiashara yeyote atakayeibuka mshindi atapaswa kulipia asilimia ishirini na tano (25%) ya bei papo hapo na asilimia sabini na tano (75%) italipwa yote katika muda wa siku kumi na nne (14) baada ya mnada.

Kufuatia sharti hilo baada ya kutangazwa kwa mshindi,  Mwakilishi kutoka Kampuni hiyo, Grey Kilas   aliweza kulipia asilimia ishirini na tano (25%) papo hapo na asilimia sabini na tano (75%) ataimalizia   ifikapo Februari 11, 2018.

Wakati huohuo,  Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu TAWA, Mabula Misungwi amewatoa wasiwasi wananchi kuwa biashara hiyo haiwezi kuchochea ujangili kwa vile meno hayo yanauzwa kwa wafanyabiashara wale tu wenye leseni za nyara daraja la kwanza.

Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa meno hayo, Misungwi amesema meno hayo yanatokana na vifo vya asili pamoja na uthibiti wa wanyamapori waharibifu katika kulinda na kuokoa mali za wananchi.

Kwa upande mwingine, Misungwi amesema kuwa uuzaji huo wa nyara hizo uko kwa mujibu wa kifungu cha 88 cha sheria ya kuhifadhi wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 (Sura 283)
 

Aidha, Misungwi alisema meno hayo yalianza kukusanywa tangu mwaka 2004 na huko nyuma serikali ilikuwa ikiyauzia makampuni yenye leseni lakini kwa mwaka hu wameanzisha utaratibu mpya kwa kuyauza kwa njia ya mnada.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Kampuni iliyofanikiwa kununua meno hayo , Grey Kilas amewashukuru wasimamizi wa mnada huo kuwa umeendeshwa kwa uwazi wa hali ya juu na umetoa fursa kwa kila mmoja wao na hatimaye yeye kuibuka mshindi.

Akizungumzia kuhusu soko, Kilasi amesema meno hayo huuzwa nchini Japan, Marekani na Hongkong ambapo hutumika katika kutengenezea mapambo kama vile stempu, sanamu pamoja na vishikizo vya nguo.

Itakumbukwa kuwa kwa mara mwisho biashara hiyo ya kuuza meno ya viboko ilifanyika mwaka 2004.

 

 

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top