You Are Here: Home » Whats New » SERIKALI YAPIGA MARUFUKU UCHOMAJI MATOFALI KWA KUTUMIA NISHATI YA KUNI

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU UCHOMAJI MATOFALI KWA KUTUMIA NISHATI YA KUNI

Serikali imepiga marufuku uchomaji matofali kwa njia ya tanuri kwa kutumia nishati ya kuni hasa katika maeneo ya mijini na badala yake imewataka wachomaji hao watumie pumba kama nishati mbadala ya kuchoma matofali hayo.

Onyo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu wakati alipokuwa akizungumza na kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Geita ikiwa ni ziara yake kwanza ya kikazi kwa mikoa ya Kaskazini Magharibi tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo.


Amesema uchomaji matofali kwa kutumia nishati ya kuni umekuwa ukichangia upotevu mkubwa wa misitu hali inayotishia sehemu kubwa ya nchi kuwa jangwa.

Amefafanua kuwa matofali yachomwe kwa kutumia pumba za mazao badala ya kuni hali itakayopelekea kunusuru nchi kuwa jangwa huku akiagiza kamati hiyo ya mkoa huo kuanza kulisimamia agizo hilo mara moja.


Amesema sehemu kubwa ya nchi kwa sasa uharibifu wa mazingira umeongezeka kufuatia ukataji miti ovyo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo uchomaji wa matofali kwa kutumia kuni.

“Mimi sipo tayari kuona nchi inageuka kuwa jangwa lazima nisimamie kwa kuanza katika maeneo ya mjini kama vile Geita unakutana na tanuri za kuchoma matofali kwa kutumia kuni, hili sikubaliani nalo” amesisitiza Mhe.Kanyasu

Amesema kwa mujibu wa takwimu Tanzania imekuwa ikipoteza zaidi ya hekta 372,000 za misitu nchini kila mwaka.

Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu ameiagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) ihakikishe inasimamia ipasavyo mipaka mipya ya baadhi ya misitu ya Hifadhi katika mkoa Geita ambayo imehaulishwa kwa kuhakikisha imetangazwa kwenye gazeti la serikali.

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top