You Are Here: Home » Whats New » SERIKALI YAJIPANGA KUIMARISHA UTALII WA FUKWE

SERIKALI YAJIPANGA KUIMARISHA UTALII WA FUKWE

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa amesema Serikali itajizatiti kuboresha fukwe ili ziweze kuwa vivutio vya utalii nchini kwa lengo la kuongeza mapato yatokanayo na sekta ya Utalii.


Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Oktoba 12, 2018) wakati alipomuwakilisha Rais Dkt. John Magufuli kwenye ufunguzi wa onesho la Kimataifa la Utalii la Swahili International Tourism Expo, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar ES Salaam.

Onesho hilo linalofanyika kwa siku tatu nchini linahudhuriwa na wafanyabishara wakubwa wa utalii takriban 170 kutoka nchi mbalimbali duniani pamoja na wauzaji wa bidhaa za utalii takriban 300 kutoka ndani na nje ya nchi.


Waziri Mkuu amesema sekta ya utalii nchini inachangia zaidi ya asilimia 25 ya mauzo yote ya nje na takriban ajira 1,500,000, ambapo kati ya ajira zote za moja kwa moja na zile ambazo si za moja kwa moja.


Amesema kutokana na juhudi za utangazaji wa vivutio vya utalii nchini unaoratibiwa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), wageni wengi maarufu duniani wanakuja kuona vivutio hivyo wakijua kwamba Tanzania ni nchi ya amani, yenye utulivu na Watanzania ni watu wakarimu.


Amesema kati ya wageni hao waliokuja hapa nchini kwa mwaka huu ni pamoja Rais Mstaafu wa Marekani, Bw. Barack Obama aliyekaa siku nane; Rais wa Uswisi Bw. Alain Berset aliyekaa siku 10 pamoja na mchezaji wa golf mstaafu kutoka Marekani, Bw. Jack Nicklaus.


Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa mbali na watu hao maarufu duniani kuja nchini pia makundi makubwa ya watalii yenye zaidi ya watu 300, wameingia nchini tangu mwanzoni mwa mwaka huu kutoka nchi za Israel, Australia na Hispania. “Hii ni ishara njema kwa maendeleo ya kasi ya sekta hii.”


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Japhet Hasunga amemshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa mchango wake mkubwa kwenye maendeleo ya sekta ya utalii nchini kutokana na hatua mbalimbali anazozichukua katika kukuza sekta hiyo.


Amesema miongoni mwa hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli katika kuimarisha sekta ya utalii ni pamoja na kuboresha usafiri wa anga nchini, ambao kwa sasa umeongezeka kwa sababu ya uwekezaji mkubwa wa Serikali.


Ameongeza kuwa utalii ni sekta mtambuka inayomgusa kila mwananchi hivyo Wizara inaendelea kuweka mazingira bora zaidi ili iweze kumgusa kila mwananchi kimapato.


Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof.Adolf Mkenda amesema sekta ya utalii ina mchango mkubwa hata hivyo mchango wake utakuwa maradufu kama uwekezaji wa kumbi za kimataifa utaimarishwa ili kuwavutia watalii


Amefafanua kuwa watalii walio wengi hawaji nchini kwa ajili ya kupumzika pekee bali wanakuja wakiwa wameunganisha kufanya shughuli maalum hivyo kuna haja kubwa ya kuwekeza kwenye utalii wa mikutano ili kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini.

 

 

 

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top