You Are Here: Home » Whats New » SERIKALI KUNYANG’ANYA HOTELI ILIZOZIBINAFSISHA KWA WAWEKEZAJI

SERIKALI KUNYANG’ANYA HOTELI ILIZOZIBINAFSISHA KWA WAWEKEZAJI

Serikali imeanza ukaguzi wa hoteli za Kitalii ilizozibinafsisha kwa Wawekezaji na wale watakaobainika kuziendesha chini ya kiwango, watanyang'anywa na kupewa wawekezaji wengine walio tayari kuziendesha kwa manufaa ya kukuza utalii nchini.


Hatua hiyo inafanyika kufuatia kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa watalii na wadau mbalimbali wa utalii juu ya huduma zisizoridhisha zinazotolewa na hoteli hizo.

Akizungumza mara baada ya kukagua baadhi ya hoteli za Kitalii ikiwemo ya   Soronera na Lobo, zilizo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe Constantine Kanyasu amesema lengo la kubinafsishwa kwa Hoteli hizo ilikuwa ni kuboresha huduma.

Pia,  Hoteli ya Musoma ya mkoani Mara pamoja na Ngorongoro Wildllife iliyopo ndani ya Mamlaka ya Eneo la Ngorongoro ni miongoni mwa hoteli   zilizofanyiwa ukaguzi.

Amesema Mwekezaji asiyefanya hivyo atanyang’anywa umiliki ili apewe mwekezaji   mwingine mwenye uwezo wa kutoa huduma bora.

Aidha, amesema kumekuwa na tuhuma kwa baadhi ya hoteli zilizobinafsishwa kukwepa kodi ya tozo ya huduma pamoja kuwalipa wafanyakazi wazawa mishahara midogo huku wale wa kigeni wakilipwa mishahara mikubwa kwa kazi ya aina moja.

Mhe. Kanyasu amesisitiza kuwa, Serikali ilizibinafsisha hoteli hizo ili zilete mapinduzi katika nyanja ya ajira, huduma bora kwa watalii, kodi pamoja kuziboresha ili zikidhi soko la watalii kwa sasa.

Akizungumza mara baada ya kukagua hoteli hizo,Mhe Kanyasu amebainisha baadhi vitu alivyoviona ikiwemo uchakavu wa miundombinu pamoja na udanganyifu wa idadi ya watalii wanaofikia katika hoteli hizo .

Amesema Wizara itapeleka idadi ya hoteli zitakazobainika kwenda kinyume ili Msajiri wa Hazina aweze kuzifutia umiliki.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kanyasu amewataka viongozi wa Hoteli hizo kukaa na kuona ni namna watakavyoongeza idadi ya Watanzania wanaotembelea hifadhi na kupata mapumziko katika Hoteli hizo.

Kuhusu Tozo ya huduma ya Mapato amezielekeza Halmashauri mbalimbali ikiwemo ya Serengeti kupata taarifa sahihi kutoka Hifadhi za Taifa ( TANAPA)

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti,  Victor Tonesha amesema changamoto inayoikabili Halmashauri hiyo ni ya kushindwa kubaini kiwango halisi cha fedha zinazotolewa na Wawekezaji hao.

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top