You Are Here: Home » Whats New » NAIBU WAZIRI, MHE.KANYASU ATAKA USHIRIKISHWAJI UTATUZI MIGOGORO HIFADHINI

NAIBU WAZIRI, MHE.KANYASU ATAKA USHIRIKISHWAJI UTATUZI MIGOGORO HIFADHINI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu ameitaka Taasisi ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, (TAWA) iwashirikishe wananchi pale inapotokea migororo ya ardhi kati ya Hifadhi na wananchi.

Amesema lengo la ushirikishwaji huo ni kujenga mahusiano mazuri   kati ya Wananchi na Hifadhi ambao ndio walinzi wakubwa wa Hifadhi.

Mhe.Kanyasu ametoa rai hiyo wakati akizungumza na watumishi wa TAWA katika ofisi za makao makuu mkoani Morogoro ikiwa ni mara yake ya kwanza kukutana na watumishi hao tangu alipoteuliwa kushika wadhifa huo katika Wizara hiyo nyeti kwa uchumi wa nchi.

Amesema ziara yake imelenga kuzifahamu Taasisi anazoziongoza ili kujua namna zinavyotenda kazi na changamoto zinazowakabili ili kuzipatia ufumbuzi.

Pia, Ameitaka TAWA Ijiepushe na matumizi ya mabavu badala yake ijikite zaidi kwenye mazungumzo baina ya wananchi ili kujenga ushirikiano endelevu katika shughuli za uhifadhi.na jamii zinazunguka maeneo yao.

‘’Moja ya mipango ya Wizara ni kuhakikisha migogoro yote ya ardhi inayowezekana inatatuliwa haraka iwezekanavyo ’’ Alisisitiza Mhe. Kanyasu

Sambamba na hilo, Mhe. Kanyasu ameishauri TAWA kuwa na programu maalumu ya kushughulikia tatizo la uingizwaji mifugo hifadhini badala ya kuendesha operesheni ambazo zimekuwa na matokeo ya muda mfupi.

Amefafanua kuwa Operesheni hizo haziwezi kumaliza tatizo la mifugo katika Hifadhi kwa vile zimekuwa zikifanyika ndani ya kipindi cha muda mfupi baada ya hapo wafugaji huingiza tena mifugo hifadhini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAWA, James Wakibara amesema tabia ya wafugaji kuingizaji mifugo katika mapori ya Akiba   imekuwa ikiigharimu Taasisi hiyo kwa kutumia fedha nyingi pamoja na muda

Amesema mfano kwa mwaka jana, Askari wanyamapori katika maeneo mengi ya Mapori ya Akiba walitumia muda mwingi kulinda mifugo iliyokamatwa Hifadhini.

Ameongeza kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha uhasama katika ya wafugaji na taasisi hiyo kwa vile mifugo mingi iliyokamatwa hifadhini hufa na mingine huugua wakati ikisubili kumalizika kwa kesi mahakamani kwa vile Askari wanyamapori sio wataalamu wa ng’ombe.

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo, Dkt. Wakibara amesema kufuatia ushauri alioutoa Mhe. Kanyasu wa kuunda Program maalum na endelevu ya kushughulikia mifugo hifadhini baadala kuendesha operesheni anaamini mara baada ya kuiunda programu hiyo itakuwa na tija katika kumaliza tatizo hilo.

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top