You Are Here: Home » Whats New » NAIBU WAZIRI KANYASU AWAHAMASISHA WABUNGE KUTEMBELEA VIVUTIO VYA UTALII

NAIBU WAZIRI KANYASU AWAHAMASISHA WABUNGE KUTEMBELEA VIVUTIO VYA UTALII

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu amewataka Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa chachu ya kuhamasisha utalii wa ndani kwa wananchi wanawaongoza kwa kutenga muda wa kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Imeelezwa kuwa hamasa ya wananchi ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini imekuwa na mwitikio mdogo ukilinganisha na idadi ya watalii wa kutoka nje.

Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu akiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakati Kamati hiyo ilipofanya ziara ya siku mbili ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa mradi wa kukuza na kuendeleza utalii Kusini katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha mkoani Iringa.

Amesema endapo kila Mbunge kwa nafasi yake ataweza kuhamasisha wananchi kutembelea vivutio vya utalii mapato yataweza kuongeza maradufu kupitia Utalii wa ndani tofauti na ilivyo sasa.

“Tengeni muda wa kupumzika baada ya pilikapilika ya kuwahudumia wapiga kura wenu, unakuja huku Ruaha unapumzisha akili huku ukijipanga mwaka 2020 kwa ajili ya uchaguzi Mkuu” alisema.

” Tusisubiri tuje kikazi kama tulivyokuja hivi, Panga njoo na familia yako ufurahie maisha mara moja moja sio mbaya” Alisisitiza Kanyasu.

Pia, Kanyasu aliwaomba Wabunge hao kila wanapopata nafasi ya kukutana na wananchi majimboni mwao wawahamasishe kutembelea vivutio vya utalii ili kumuunga mkono Rais John Magufuli kwa jitihada anazofanya za kutaka kuongeza mapato yatokanayo na sekta ya utalii.

Amesema ufufuaji wa kampuni la usafiri wa ndege nchini (ATCL) kwa kununua ndege saba achilia mbali mradi wa reli ya Standard Garge ni juhudi wazi za Rais John Magufuli kuona sekta ya utalii inagusa maisha ya kila wananchi kimapato.

Katika hatua nyingine, Kanyasu aliwaomba Wabunge hao wawahamasishe wananchi kuchangamkia fursa za utalii kwa kujenga Hoteli au kwa kuanzishavituo vya utalii wa kiutamaduni ambao umekuwa ukipendwa sana na watalii wengi wa kutoka nje.

Aidha, Mhe.Kanyasu aliwaeleza Wabunge hao kuwa baada ya kufungua utalii Kusini, Serikali inakusudia kufungua utalii katika kanda nyingine ikiwemo ya kanda ya ziwa na kanda ya Kaskazini Magharibi, Hivyo wawaandae wananchi wao kuchangamkia fursa za utalii badala ya kubaki walalamikaji.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mtama ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Nape Nnauye alisema kufunguliwa mapema kwa utalii Kusini kutatoa picha halisi kwa wananchi katika kunufaika kiuchumi kupitia sekta hiyo katika kanda nyingine

Pia, Mhe, Nape aliishauri Serikali kulifanyia kazi suala la tozo ya kuingia ndani ya hifadhi (single entry) kutokana na malalamiko ya muda mrefu wanayoyatoa wananchi kwanaoishi Katibu na Hifadhi kuwa imekuwa ikiwabana watalii kutoka nje ya Hifadhi kuwatembelea wananchi hao.

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top