You Are Here: Home » Whats New » NAIBU WAZIRI KANYASU AWAFUNDA WAHITIMU WA JESHI USU KUHUSU MALIASILI

NAIBU WAZIRI KANYASU AWAFUNDA WAHITIMU WA JESHI USU KUHUSU MALIASILI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Costantine Kanyasu amewataka askari wa misitu waliohitimu mafunzo ya kijeshi kuhakikisha wanarejesha uoto wake wa asili katika maeneo yote ya misitu ambayo yameharibiwa.


Mhe. Kanyasu ameya sema hayo wakati alipokuwa akifunga mafunzo ya kijeshi kwa askari 140 wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika kambi ya mafunzo ya kijeshi Mlele mkoani Katavi.

“Leo mmehitimu na tumewaapisha, mmekuwa askari kweli wa TFS lakini tambueni kuwa kazi za kiuchumi zinapelekea uharibifu mkubwa sana wa mazingira, na hatuwezi kusema zisiendelee! Zinatakiwa kuendelea katika namna ambayo haitaifanya nchi yetu kuwa jangwa.

“Kuhitimu kwenu hakumaanisha mnakwenda kuzuia maendeleo, kunamaanisha mnakwenda kushirikiana na wanaotaka maendeleo kwa kufanya kazi wakifikiria maendeleo endelevu,” anasema.

Amesema kwa sasa nchi inakabiliwa na mabadiliko makubwa ya tabia nchi yanayosababishwa na uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti, ukame, mvua nyingi na mafuriko ambapo vyote hivyo husababishwa na matumizi mabaya ya kazi za kiuchumi.

Amesema ni matarajio ya Serikali baada ya askari hao kuhitimu pamoja na kazi yao ya msingi ya ulinzi watafanya kazi ya kuhakikisha wanarejesha uoto wa asili uliopotea.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Prof. Dos Santos Silayo katika hotuba yake amesema Taifa limekuwa likikumbwa na changamoto mbalimbali za kiuhifadhi ikiwemo shughuli za kibinadamu pamoja na mmomonyoko wa maadili kwa watumishi na mambo yote hayo yanapelekea mafunzo hayo kuwa muhimu katika uhifadhi wa mapori na misitu ya hifadhi nchini.


Pia, Prof. Silayo amesema pamoja na mafunzo hayo yanayofanyika,  TFS inaimarisha vikosi vyake vya kufuatilia taarifa ambapo ina kitengo cha intelejensia ambacho wanakiimarisha ili kiweze kutoa taarifa sahihi kwa askari wa misitu na kuchukua hatua bila kupoteza wakati.


Zoezi hilo limehudhuriwa na viongozi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili,  na Utalii pamoja na wananchi.


Wizara ya Maliasili na Utalii imebadili mfumo wake wa usimamizi wa maliasili toka ule wa kiraia kwenda mfumo wa kijeshi (Paramilitary). TFS imekuwa mstari wa mbele kwenda na mabadiliko hayo kwa kuanza kutekeleza mafunzo ya watumishi katika ngazi mbalimbali wakati ikisubiri mabadiliko ya muundo wa utumishi utakaotambua mabadiliko ya vyeo na majukumu ya kila siku.

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top