You Are Here: Home » Whats New » MAKUMBUSHO MPYA YA OLDUVAI YAWAFURAHISHA WABUNGE, NAIBU WAZIRI

MAKUMBUSHO MPYA YA OLDUVAI YAWAFURAHISHA WABUNGE, NAIBU WAZIRI

Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kazi nzuri iliyofanya ya ujenzi wa jengo la makumbusho ya kisasa katika Bonde la Olduvai ya Gorge ambako ni chimbuko la historia ya Binadamu

Kamati hiyo imesema imeridhishwa na ujenzi wa jengo hilo ambalo litawavutia watalii na wanasayansi wabobezi wa masuala ya Malikale kutembelea Makumbusho hiyo.

Akitoa pongezi za kamati hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Kemilembe Luota alisema kuwa mbali ya Makumbusho hiyo   kutumika kuingiza pesa kupitia watalii pia inatumika kama kielelezo na utambulisho muhimu wa taifa katika kutangaza utamaduni wa Mtanzania ndani na nje ya nchi.

Luota alisema hayo juzi wakati kamati hiyo ilipofanya ziara ya kutembelea Ngorongoro Crater na Makumbusho ya Olduvai Gorge katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Mwenyekiti aliwapongeza wataalamu kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa kuhakikisha kuwa eneo la Olduvai Gorge linakuwa kivutio bora kwa ajili ya historia ya nchi na kivutio kikubwa cha Utalii duniani.

‘’ Sisi kama Kamati tunaipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kuyafanyia kazi mapendekezo yote tuliyoyatoa kwa mara ya kwanza tulipokuja kwa vile tumeona kazi nzuri imefanyika.’’

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo ametoa wito kwa wananchi kutembelea makumbusho hiyo kwa vile idadi ya watalii wa ndani aliyokutana nayo sio ya kuridhisha.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga amesema makumbusho hiyo inatoa ushahidi dhahiri kuwa hata wazungu, mababu zao walitoka Afrika.

Mjumbe wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Mtama,  Nape Nnauye amesema Makumbusho hiyo hadi hapo ilipofikia imeboreshwa kwa kiwango cha hali ya juu hata hivyo ameitaka Wizara ihakikishe inaitangaza ipasavyo ili watalii wengi zaidi wazidi kutembelea.

Awali, Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka hiyo, FredyManongi amesema tangu kuzinduliwa kwa makumbusho hiyo kwa wiki moja imekuwa ikipokea zaidi ya watalii wapatao 40000 hali inayopekelea   kuwa ni miongoni mwa Makumbusho inayofanya vizuri zaidi barani Afrika

 

 

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top