You Are Here: Home » Whats New » HIFADHI YA MIKUMI YAIOMBA SERIKALI KUCHEPUSHA NJE BARABARA YA LAMI INAYOPITA HIFADHINI

HIFADHI YA MIKUMI YAIOMBA SERIKALI KUCHEPUSHA NJE BARABARA YA LAMI INAYOPITA HIFADHINI

HIFADHI YA MIKUMI YAIOMBA SERIKALI KUCHEPUSHA NJE BARABARA YA LAMI INAYOPITA HIFADHINI


Na Hamza Temba-WMU-Morogoro

................................................................

Serikali inafikiria namna bora ya kubadilisha
uelekeo wa eneo la kilometa hamsini za barabara ya lami inayopita ndani ya
Hifadhi ya Taifa ya Mikumi au kutoza kodi ya utalii kwa watu wanaotumia
barabara hiyo ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazosabishwa na
barabara hiyo kwenye uhifadhi.Hayo yamesemwa mkoani Morogoro na
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla kufuatia ombi la uongozi
wa hifadhi hiyo la kuiomba Serikali kuchepusha barabara hiyo kutokana na athari
mbalimbali za kimazingira zinazosabishwa na uwepo wa barabara hiyo ndani ya
hifadhi hususan vifo vya mara kwa mara vya wanyamapori, ujangili na ukosefu wa
mapato ya Serikali.


Awali akiwasilisha taarifa ya hifadhi
hiyo mbele ya Waziri Kigwangalla, Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Gerald
Mono alisema licha ya barabara hiyo kuwa na fursa nyingi za kimaendeleo imekuwa
na changamoto nyingi kwenye uendeshaji wa shughuli za uhifadhi.


Alisema wastani wa mnyamapori mmoja
hugongwa na gari kila siku katika barabara hiyo ambapo takwimu zinaonyesha kuwa
mwaka 2014 idadi ya wanyamapori waliogongwa walikuwa 351, mwaka 2015 walikuwa 361
na mwaka 2016 walikuwa 218.


Alisema changamoto nyingine ni
uchafuzi wa mazingira ambapo wastani wa taka ngumu zisizopungua kilo 138.3
huzalishwa kila siku na watumiaji wa barabara hiyo.


Mbali na changamoto hizo alisema nyingine
ni ukosefu wa mapato ya Serikali kufuatia kukosekana kwa mageti ya kulipia tozo
za utalii kwa watumiaji wa barabara hiyo ambao hufaidi utalii wa bure na
kuikosesha Serikali mapato.


Alisema Changamoto nyingine ni
ujangili ambao huchochewa na uwepo wa barabara hiyo ambayo hutoa fursa kwa
majangili kuingia katika hifadhi hiyo kiurahisi kwa njia mbalimbali ikiwemo
magari na pikipiki.


“Hifadhi inaiomba Serikali kuchepusha
barabara hii ili kupunguza changamoto hizi zinazotokana na uwepo wa barabara
husika na kuongeza mapato ya Hifadhi kwa kuzuia utalii a bure unaofanywa na
watumiaji wa barabara wa ndani na nje,”. Alisema Kaimu Mhifadhi Mkuu huyo wa
Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.


Kwa upande wake Waziri wa Maliasili
na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla alisema changamoto kubwa aliyoiona katika
hifadhi hiyo ni namna ya watalii kufika na kufanya shughuli za utalii katika
hifadhi hiyo.


Alisema licha ya uwepo wa barabara ya
lami inayokatiza hifadhini hapo, barabara hiyo sio rafiki kwenye uhifadhi. “Kuna
hiyo barabara ambayo inaleta watalii hapa, ni barabara ambayo iko bize sana, ni
barabara ya kitaifa na kwa vyovyote vile hii sio barabara mahsusi kwa ajili ya
shughuli za utalii.


“Sisi (Serikali) tunatafakari namna ya aidha
kuiondoa hiyo barabara au namna ya kuwachaji watu wanaokatiza hizi kilometa
hamsini ambazo zipo ndani ya hifadhi ya Mikumi,” alisema Dk. Kigwangalla.


Katika hatua nyingine Dk. Kigwangalla
amemtaka muwekezaji aliyepewa hoteli ya kitalii ya Mikumi Wildlife Lodge
iliyopo ndani ya hifadhi hiyo kwa ajili ukarabati na uendelezaji kuhakikisha anakamilisha
makubaliano hayo ndani ya muda aliyopewa kwa mujibu wa mkataba aliosaini na TANAPA
ama sivyo atanyang’anywa kibali hicho.


Akizungumzia jitihada za kuimarisha
ulinzi wa hifadhi hiyo, Dk. Kigwangalla amesema Serikali inakusudia kuharakisha
mchakato wa kuanzishwa kwa jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori ya Kidoma
itakayojumuisha vijiji vya Kilangali, Doma na Maharaka ili kutengeneza buffer
na hatimaye kuimarisha uhifadhi shirikishi.


Hifadhi ya Taifa ya Mikumi
ilianzishwa mwaka 1964 kwa Tangazo la Serikali Na. 465 ikiwa na ukubwa wa
kilometa za mraba 1,070. Mwaka 1975 Serikali iliona umuhimu wa kuongeza eneo
upande wa kusini na kaskazini mwa Hifadhi na kufikia ukubwa wa kilometa za
mraba 3,230 kwa tangazo la Serikali Na. 121.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi
Kigwangalla akiongea na Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi,
Gerald Mono wakati wa ziara yake ya kikazi katika hifadhi hiyo jana mkoani
Morogoro. Uongozi wa hifadhi hiyo umeiomba Serikali kuchepusha barabara ya lami
inayopita ndani ya hifadhi hiyo kutokana na athari mbalimbali za kimazingira
zinazosabishwa na barabara hiyo ikiwemo vifo vya wanyamapori, ujangili na
ukosefu wa mapato ya Serikali unaotokana na watu kufaidi utalii wa bure. 

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi
Kigwangalla akikagua maziringira ya jengo lililoungua moto la Mikumi Wildlife
Lodge ambalo linalofanyiwa ukarabati wakati wa ziara yake ya kikazi katika Hifadhi
ya Taifa ya Mikumi jana mkoani Morogoro ambapo amemtaka muwekezaji aliyepewa
hoteli hiyo kuikarabati ndani ya muda aliopewa ama sivyo atanyang’anywa kibali alichepewa.
Kushoto kwake ni Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Gerald Mono. 


Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi
Kigwangalla akiongozwa
 na Kaimu Mhifadhi
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Gerald Mono kukagua mazingira ya hifadhi
hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi katika hifadhi hiyo jana mkoani Morogoro. 

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akipata maelezo  kutoka kwa Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Gerald Mono wakati wa ziara yake ya kikazi katika hifadhi hiyo jana mkoani Morogoro.

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiangalia mazingira mwanana ya  Hifadhi ya Taifa ya Mikumi wakati wa ziara yake ya kikazi katika hifadhi hiyo jana mkoani Morogoro.

Picha ya pamoja.

 

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top