You Are Here: Home » Whats New » FARU 12 KUINGIZWA NCHI

FARU 12 KUINGIZWA NCHI

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na utalii Prof.Adolf Mkenda amesema kuwa Taasisi isiyo ya kiserikali ya Grumeti Fund inatarajia kuingiza faru 10 nchini kwa ajili kuongeza idadi ya wanyama hao hapa nchini.

Kuagizwa kwa Faru hao kutaongeza idadi yao kutoka 2 walioagizwa na taasisi hiyo hapo awali hadi kufikia 12.

 

Akizungumza katika kikao kilichowahusisha wadau hao wa uhifadhi kilichofanyika katika chuo cha Uhifadhi wa Wanyamapori cha Pasiansi jijiji mwanza, Prof. Mkenda amewashukuru wadau hao kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha shughuli za uhifadhi nchini. 

Amesema Serikali itaendeleza mahusiano mazuri yaliyopo baina yake na wadau wote wapenda maendeleo kwa lengo la kulinda na kukuza shughuli za uhifadhi wa wanyamapori nchini.

Prof. Mkenda amesema kuwa kuletwa kwa faru hao kutaongeza idadi ya wanyama hao hapa nchini na kuongeza kuwa taasisi ya Grumeti imesaidia kuwaleta watu maarufu kutoka katika mataifa mbalimbali kuja kutembelea hifadhi za Taifa na hivyo kuchangia kutangaza utalii na kuongeza pato la Taifa.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa idara ya wanyamapori Tanzania Canisius Karamaga akizungumzia kuhusu ujio wa Faru hao amesema kuwa jitihada zinazofanywa na taasisi hiyo zinalenga kuwaongeza Faru hao hapa nchini.

Ameongeza kuwa Faru hao wataingizwa nchini kwa lengo la kuboresha kizazi cha wanyama hao waliokuwa hatarini kutoweka ikiwa ni moja ya juhudi za kuwafanya waongezeke kwa kuzaliana na wale waliopo nchini.

Amesema kikao hicho kati ya wizara na wadau hao ni muhimu sana kwa kuwa kimejadili na kuangalia kwa utalaam Zaidi namna Faru hao watakavyoingizwa nchini, kutunzwa na kulindwa kwa kuwa wanyama hao ni adimu na muhimu kwa utalii.

Amewataka watanzania kuwa mstari wa mbele kulinda rasilimali za nchi ili ziwe na faida kwa vizazi vijavyo.

 

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top