You Are Here: Home » Whats New » WIZARA YAENDELEA KUKUSANYA MAONI YA KUBORESHA SERA YA TAIFA YA UTALII KWA WADAU WAKE

WIZARA YAENDELEA KUKUSANYA MAONI YA KUBORESHA SERA YA TAIFA YA UTALII KWA WADAU WAKE

Wizara ya Maliasili na Utalii imewataka Wadau wa Sekta ya Utalii wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kutoa maoni na michango yenye tija itakayopelekea upatikanaji wa Sera Mpya ya Utalii.

Sera hiyo   inatarajiwa kutoa majibu ya changamoto za utalii wa sasa kwa sababu itagusia utalii nje ya hifadhi.

Kauli hiyo imekuja baada ya Sera ya Taifa ya Utalii inayotumika hadi hivi sasa kufanyiwa mapitio kwa mara ya mwisho mwaka 1999 ambapo ni takribani miaka 17 iliyopita. 
Hayo yameibainika kwenye warsha ya siku moja iliyoandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii na kuwatanisha wadau wa sekta hiyo wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ili kukusanya maoni ya upungufu na utekelezaji wake.

Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Zahoro Kimwaga alisema Sera na miongozo inayoongoza Sekta ya utalii imepitwa na wakati kutoka na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii yaliyotokea mfano, Serikali kujiondoa katika umiliki na uendeshaji wa huduma za kitalii na kuachia sekta binafsi.

’’Si hayo tu sera ya awali haikuainisha vivutio vyote vya utalii zaidi ya hifadhi pekee ambapo kwa sasa tatizo la ujangili na mabadiliko ya tabia nchi yameathiri kwa kiasi kikubwa’’ alisema

Aliongeza kuwa, Sera mpya itakayoundwa itaweza kwenda sambamba na aina ya utalii wa sasa ambao kipindi cha nyuma haukuwepo, akitolea mfano utalii mikutano pamoja na utalii wa kiutamaduni ambao umekuwa ukikua kwa kasi hapa nchini

Aidha, alifafanua kuwa wanahitaji miongozo mipya itakayosimamia sekta hiyo ili kuondoa migongano ya kiutendaji katika taasisi zinazohusika ikiwemo ya wanyamapori, misitu na uwekezaji ili kuendeleza utalii na sio kudidimiza.

Akifungua warsha hiyo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Fikira Kisimba allisema wameamua kupitia sera hiyo kutokana na kasi ndogo ya maendeleo yanayopatikana katika sekta hiyo licha ya kujaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii.

Kwa upande wake, Afisa Utalii wa Mkoa wa Njombe, Amiri Abdi, alisema sera itakayoundwa iangalie namna ya kuweza kutumia teknolojia rafiki ya kuvitangaza vivutio vya vya Utalii vya Nyanda za Juu Kusini kwa kutumia gharama nafuu.

 

 

 

 

 

 

© 2018 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top