You Are Here: Home » Whats New » WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAPOKEA VITENDEA KAZI KUTOKA USAID

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAPOKEA VITENDEA KAZI KUTOKA USAID

WIZARA ya Maliasili na Utalii imepokea vifaa mbalimbali vya mawasiliano vyenye thamani ya shilingi milioni 34,936,400 kutoka Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani kupitia mradi wa USAID PROTECT ili kusaidia katika kukuza uelewa wa wananchi kuhusu uhifadhi endelevu wa Maliasili, Malikale na Uendelezaji Utalii kwa manufaa ya Tanzania na dunia kwa ujumla.

Akizungumza leo katika hafla fupi ya makabidhiano ya vifaa hivyo iliyofanyika katika ukumbi mikutano wa makao makuu ya Wizara hiyo jijini Dodoma,  Mshauri wa Masuala ya Mazingira kutoka USAID,  Karolyn Upham ameishauri Wizara hiyo kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika   kwa lengo lililokusudiwa.

Amesema ushirikiano uliopo baina ya Tanzania na Marekani umewezesha kuwepo kwa ushirikiano wa karibu katika kuendeleza masuala mbalimbali ya maendeleo hapa nchini ikiwemo uhifadhi endelevu na uendelezaji utalii.

Ametaja vifaa hivyo kuwa ni kompyuta 10, kamera tano, printa tatu, skana mbili, fotokopi mashine mbili, TV pamoja na king’amuzi.

Mbali na vifaa hivyo USAID itatoa mafunzo kwa Menejimenti ya Wizara kuhusu namna bora ya kuwasiliana na Umma (Effective public communication) itaboresha tovuti ya Wizara,  itachapa vipeperushi 6000 ikiwa ni pamoja na kupitia mkakati wa Mawasiliano wa Wizara.

Msaada huo kutoka USAID ukiunganisha thamani ya vifaa vilivyotolewa pamoja na mafunzo yatakayotolewa itagharimu jumla ya shilingi milioni 100.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Iddi Mfunda amesema,  “Tumepewa jukumu la kusimamia maliasili,  malikale pamoja na kuendeleza utalii nchini hivyo tutahakikisha tunatekeleza jukumu hilo kikamilifu”

Ameongeza kuwa, Kupatikana kwa vifaa hivyo kutaongeza tija katika utendaji wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini.

Naye, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,  Dorina Makaya amesema vifaa hivyo vitachangia katika kukiwezesha Kitengo cha Mawasiliano kufanya kazi kwa wepesi zaidi kwenye utoaji wa taarifa kwa umma kwa lengo la kukuza uelewa wa wananchi katika uhifadhi endelevu na uendelezaji utalii kwa manufaa ya taifa na dunia kwa ujumla.


Akizungumza wakati wa kufunga hafla hiyo,  Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara hiyo,  Bibi Esther Kazenga ameelezea kutambua juhudi za USAID katika kuunga mkono juhudi za Serikali katika nyanja mbalimbali za maendeleo na amewaomba USAID kuendelea kuunga mkono juhudi za Wizara katika kuinua uelewa wa wananchi na ushiriki wao katika Uhifadhi na Uendelezaji Utalii kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.


 

 

 

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top