You Are Here: Home » Whats New » WAZIRI KANYASU AAGIZA MINADA YA MIFUGO ILIYOKAMATWA IFANYIKE NJE YA HIFADHI

WAZIRI KANYASU AAGIZA MINADA YA MIFUGO ILIYOKAMATWA IFANYIKE NJE YA HIFADHI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu ameagiza minada yote ya mifugo iliyokamatwa Hifadhini baada ya Serikali kushinda kesi mahamakani ifanyike nje ya Hifadhi ili kuondoa dhana mbaya iliyojengeka miongoni mwa jamii kuwa Wahifadhi hukamata mifugo hiyo ili waweze kujiuzia wenyewe.

Pia, Ameagiza minada hiyo itangazwe katika vijiji kabla ya tarehe ya kufanyika kwa lengo la kuwajulisha Wananchi hata kwa wale walioshindwa kesi hizo ili waweze kushiriki katika minada hiyo huku Mkuu wa Wilaya husika ashirikishwe ipasavyo kwenye minada hiyo.

Akizungumza na viongozi wa vijiji 15 katika kijiji cha Kisondoko ambavyo ni miongoni mwa vijiji vilivyokutwa ndani ya Pori la Akiba la Mkungunero lililopo katika wilaya ya Kondoa Mkoani Dodoma, Mhe.Kanyasu amesema minada hiyo isifanyike kwa usiri badala yake iwe wazi nje ya Hifadhi ili kutoa fursa kwa yeyote kushiriki.

Akizungumzia kuhusu ugumu wa kupata vibali vya kuingilia hifadhini wakati minada ilipokuwa ikifanyikia ndani,  Mhe.Kanyasu amesema kabla ya agizo hilo wananchi waliokuwa wakishiriki katika minada hiyo walihitajika wawe na vibali vya kuingilia hifadhini la sivyo walikuwa wakikatwa kwa kosa la kuingia hifadhini bila kibali.

Amebainisha kuwa endapo minada hiyo itafanyika kwa uwazi na nje ya Hifadhi kutasaidia kuepusha shutuma nyingi zikiwemo za rushwa zinazowakabili Wahifadhi kuwa wamekuwa wakishiriki kuwatafuta wanunuzi wa Ng’ombe kutoka mikoa ya mbali kwa makubaliano ya kulipwa mara baada ya mnada.


Amesema kitendo cha minada hiyo kuanza kufanyika nje ya Hifadhi kutasaidia kuondoa malalamiko kutoka kwa wananchi ambao wamekuwa wakidai kuwa pindi mifugo yao inapotaifishwa wamekuwa hata hawajulishwi lakini wafanyabiashara wakubwa ndo wamekuwa na taarifa.


Amesema wananchi ambao mifugo yao imekuwa ikikamatwa na baadaye kutaifishwa wamekuwa na chuki na Wahifadhi huku wakiwatuhumu kuwa wamekuwa wakishirikiana na wafanyabiashara hao kwa kuwajulisha ili wafike Hifadhini kwa ajili ya kuinunua.

Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu amewaonya askari wanyamapori wenye tabia ya kuvizia ng’ombe wakiwa mpakani kati ya kijiji na Hifadhi na kisha kuwasukumia ng’ombe hao ndani ya Hifadhi ili wazikamate kuwa vitendo hivyo havikubaliki na sio kazi waliyotumwa na Serikali.

Akizungumza mbele ya Naibu Waziri huyo, Mwenyekiti wa kijiji cha Ikengwe, Ismail Hamis amesema licha ya huo utaratibu mpya wa kufanyia minada nje ya Hifadhi, anaiomba serikali iangalie upya sheria ya kutaifisha mifugo kwani imepelekea wafugaji wengi kuwa maskini.

Ameshauri kuwa mifugo ikikamatwa ndani ya Hifadhi, waruhusiwe kulipa fidia kwa sababu mifugo hiyo ndo imekuwa tegemeo lao kwa kuwasaidia kusomeshea watoto wao.


Kwa upande wake, Naibu Kamishina wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania,( TAWA) Misungwi amemuahidi Naibu Waziri hiyo kuwa agizo lake litatekelezwa ipasavyo ili wananchi wa maeneo ya mifugo ilikokamatwa waweze kujulishwa.

Aidha, Misungwi amewataka watumishi hao kujiepusha na vitendo vya rushwa pindi wanapokamata mifugo kutoka kwa wafugaji kuwa yeyote atakayebainika atawajibishwa kikamilifu ili iwe funzo kwa wengine.

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top