You Are Here: Home » Whats New » WAZIRI ATOA WITO KWA WATANZANIA KUCHANGAMKIA FURSA YA UPANDAJI WA MITI KIBIASHARA

WAZIRI ATOA WITO KWA WATANZANIA KUCHANGAMKIA FURSA YA UPANDAJI WA MITI KIBIASHARA

Watanzania wametakiwa kutumia fursa ya upandaji wa miti kibiashara kuinua uchumi wa maisha yao na kuacha biashara haramu ya usafirishaji wa magogo nje ya nchi, badala yake watumie fursa hiyo kuzalisha bidhaa za misitu na kuziuza kwa faida zaidi.


Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe aliyasema hayo jana Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa uwekezaji wa misitu uliowashirikisha wadau wa Mazingira kutoka nchi 16 ulioandaliwa kwa ushirikiano na Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Mambo ya Nje ya Finland, Taasisi ya Uongozi na Shirika la Maendeleo ya Kifenda la Finland - FINFUND.


“Wawekezaji wa misitu wanasema wanataka soko la mazao yao na sisi tunasema soko lipo isipokuwa watengeneze bidhaa kama vitanda, viti na samani za ndani pamoja na makaratasi na vifaa vyote vinavyotokana na miti na hiyo ndiyo itawasaidia ndugu zetu kupata ajira na viwanda vitaongezeka.


“Tukiruhusu magogo kwenda nje itakuwa kama pamba yetu inalimwa hapa na kusafirishwa halafu inatengeneza nguo na tunaletewa, lazima Viwanda vijengwe na hiyo si kazi ngumu.... Tunachotaka hapa teknolojia ya viwanda ije, wasafirishe bidhaa na si magogo,” alisema Profesa Maghembe.


Aliongeza kuwa “Tunataka kufanya uwekezaji katika hewa ukaa, ambayo italeta tija kwa jamii na kutumia zaidi teknolojia katika upandaji wa miti ili kuongeza ubora na soko la mazao hayo”.


Alisema inakaridiwa kwamba hekta 30,000 za misitu zinapotea kila mwaka kutokana na sababu mbalimbali huku zikiwa zinapadwa hekta 80,000 hadi 100,000 kila mwaka.


Alisema kuna changamoto kubwa ya uchomaji mkaa na wengine wanasafirisha nje kupitia kwa bandari bubu na hivyo misitu kupotea kwa sababu pia ya uvunaji wa misitu usio endelevu.


Alisema changamoto nyingine ni uvunaji usio endelevu wa misitu na kupungua kwa vyanzo vya maji kutokana na ukataji wa miti hovyo na uharibifu wa misitu, hivyo Serikali inaongeza juhudi kuhakikisha vyanzo vya maji vinalindwa.


Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Profesa Joseph Semboja alisema jukumu lao ni kuwaweka viongozi na wadau mbalimbali katika kuangalia maendeleo endelevu ambapo kwa sasa wanaangalia namna ya kukabiliana na changamoto kubwa ya mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na kuboresha na kuendeleza misitu kibiashara.


Mwakilishi wa Benki ya Dunia, Yutaka Yoshino alisema Idara ya Misitu nchini imekuwa ikichangia ukuaji wa uchumi nchini, lakini sekta hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya tabianchi.

© 2018 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top