You Are Here: Home » Whats New » TFS YAAHIDI KUSHUGHULIKIA KERO YA USAFIRISHAJI VINYAGO KWA WATALII.

TFS YAAHIDI KUSHUGHULIKIA KERO YA USAFIRISHAJI VINYAGO KWA WATALII.

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS) yaahidi kushughulikia malalamiko ya Watalii walio wengi ambao hulazimika kuacha vinyago kwenye viwanja vya ndege walivyokuwa wamevinunua kwenye maduka mbalimbali nchini kutokana na kukosekana kwa vibali.

Hatua hiyo inakuja mara baada ya Naibu Waziri na Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu kuiagiza TFS iangalie namna bora ya kutatua tatizo hilo kwa vile limekuwa na taswira mbaya kwa nchi.

Amebainisha hilo wakati alipokuwa akizungumza kwenye mkutano na Watumishi wa makao makuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, jijini Dar es Salaam.

Amefafanua kuwa watalii wengi hununua vinyago hivyo kwenye maduka mbalimbali hapa nchini kama zawadi ya kupeleka nchini kwao lakini wanapofika kwenye viwanja vya ndege kwa ajili ya kusafiri navyo hudaiwa vibali vya kusafirisha vinyago hivyo jambo ambalo huwalazimu kuviacha kutokana na usumbufu wanaoupata.

Amesema jambo hilo limekuwa likiwafanya watalii wengi kuondoka nchini wakiwa wamekasirishwa kutokana na utaratibu huo kutokuwa wazi huku wakiamini kuwa wamedhulumiwa mali yao.

Amesema malalamiko hayo sio mazuri licha ya kuwa TFS nia yake ni njema ya kuhakikisha kuwa lazima kuwe na vibali ya kusafirishia vinyago hivyo kwa ajili uthibiti wa uharibifu wa misitu.

Amesema TFS lazima ifanye mazungumzo na taasisi nyingine ili kuweza kutatua kero hiyo ambayo imekuwa ikileta sintofahamu kwa watalii na sekta ya utalii kwa ujumla

Amesema ni rahisi kumpoteza mteja (Mtalii) lakini huweza kuchukua hata zaidi ya miaka kumi kuweza kumrudisha mteja ambaye ulikuwa umempoteza.

Amesema nia ya TFS ni njema katika kulinda misitu lakini tatizo linaloonekana ni kwamba hakuna mawasiliano thabiti kati ya TFS na Taasisi zingine kuhusiana na biashara ya vinyago.

Amesema TFS ni lazima ikae meza moja na wauzaji wa vinyago pamoja na Taasisi za uhifadhi ili waweze kutatua kero hiyo wanayokumbana nayo watalii.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo ameahidi kuwa suala hilo litafanyiwa kazi ili kuwaondolea usumbufu watalii wanaokuwa wamevinunua vinyago hivyo

Hata hivyo amesema suala la uthibiti wa usafirishaji vivyago lipo kisheria lakini kutokana na tatizo hilo atafanya mazungumzo na taasisi nyingine ili kuona namna bora ya kutatua kero hiyo.

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top