You Are Here: Home » Whats New » SERIKALI YASAINI MKATABA WA SHILINGI BILIONI 330 ZA KUENDELEZA UTALII KUSINI MWA TANZANIA

SERIKALI YASAINI MKATABA WA SHILINGI BILIONI 330 ZA KUENDELEZA UTALII KUSINI MWA TANZANIA

Serikali imesaini mkataba wa mkopo wa masharti nafuu wa dola za marekani milioni 150 sawa na shilingi bilioni 330 kutoka Benki ya Dunia kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa kuendeleza utalii kwa vivutio vilivyo katika ukanda wa kusini mwa Tanzania.

Akizungumza jana jijini Dar es Salam kabla ya kusaini mkataba huo,  Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James amesema pesa hizo zitatumika katika mradi ujulikanao kama Resilient Natural   Resource for Tourism and Growth (REGROW) utakaotekelezwa kwa muda wa miaka sita kuanzia mwaka 2017/18.

Amesema lengo la mradi huo ni kuimarisha miundombinu ya barabara yenye urefu kilometa 982, viwanja vya ndege 15, ili kuimarisha usafiri.

Pia, Katibu Mkuu Dotto James amesema pesa hizo zitatumika kununua mitambo ya ujenzi na matengenezo ya barabara pamoja na kuimarisha usafiri wa Reli kufikia Pori la Akiba la Selous, Mikumi na Udzungwa kupitia TAZARA.

Katika hatua nyingine, Amesema mradi ho utasaidia kuimarisha uwezo wa wananchi wanaoishi kando kando ya hifadhi kwa kuwajengea uwezo wa kutoa huduma za hoteli, kuongoza watalii pamoja na kutengeneza na kuuza bidhaa kwa watalii

Aidha, Amesema mradi wa REGROW utaboresha usimamizi wa matumizi ya maji ya mto Ruaha Mkuu katika Bonde la Usangu ili uweze kutiririka mwaka mzima kwa ajili ya matumizi ya wanyama hifadhini na mabwawa ya umeme ya Mtera na Kidatu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia, Bella Bird amesema mradi huo umelenga katika kuleta maendeleo kwa wakazi wa kusini kwa kuwa shughuli zote zitakazofanyika ni maendeleo ya watu.

Amesema mradi huo utasaidia katika kuinua kipato kwa wananchi wa Kusini mwa Tanzania kupitia utalii ambapo miundombinu itakayobereshwa haitatumika na watalii pekee.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi amesema mradi huo umekuja wakati muafaka kwani sekta ya utalii imeendelezwa zaidi katika ukanda wa kaskazini, huku upande wa kusini mwa nchi kukiwa na vivutio vingi lakini havijaendelezwa.

Amesema kupitia mradi huo utainua ukanda huo hali itakayopelekea Wizara kutimiza azma ya kufikia watalii milioni 8 na fedha za kigeni dola bilioni 20 kila mwaka kufikia mwaka 2025.

 

 

 

 

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top