You Are Here: Home » Whats New » SERIKALI KUBORESHA MAKUMBUSHO YA KUMBUKIZI YA NYUMBA YA MWL. NYERERE

SERIKALI KUBORESHA MAKUMBUSHO YA KUMBUKIZI YA NYUMBA YA MWL. NYERERE

SERIKALI KUBORESHA MAKUMBUSHO YA KUMBUKIZI YA NYUMBA YA MWL. NYERERE

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk.Hamisi Kigwangalla ametembelea Makumbusho ya Kumbukizi ya Nyumba ya Mwalimu Nyerere iliyopo Magomeni, Mtaa wa Ifunda Namba 62, Jijini Dar es Salaam na kuagiza kuanzishwa kwa mradi mahsusi wa kuboresha makumbusho hiyo.

Alisema mradi huo utahusisha kununua nyumba za jirani na pia kufanya mazungumzo na ofisi ya Kata ya Mzimuni, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ili kupata eneo la maegesho ya magari la kisasa, eneo la kujenga kituo cha taarifa na Maktaba, lengo ikiwa ni kuboresha mandhari ya kituo hicho iendane na uzito wa jina na heshma ya baba wa Taifa.

"Hii ni nyumba aliyoishi baba wa Taifa letu, Mwl. Julius Nyerere mwaka 1959 alipoacha kazi ya ualimu Pugu ili kupata muda zaidi wa kuendeleza harakati za kusaka uhuru wa Tanganyika. Tumedhamiria kuiboresha na kuitangaza zaidi kama kivutio muhimu cha utalii.

"Nimefika hapa leo kujionea Kituo hichi ambacho ni kielelezo kikubwa cha Mwasisi wa Taifa letu. Hapa pana hazina kubwa na kituo hiki kina mambo mengi sana ya kumuenzi Baba wa Taifa. Kwa hali tuliyoikuta kwa kweli tutakaa na timu yangu kuona tunafanya maboresho makubwa kabisa ili kiwe kama maeneo mengine ya waasisi wa Mataifa yao, kama eneo alilozaliwa Mzee Mandela kule Afrika Kusini, nyumba yake imehifadhiwa vizuri na imekuwa ikitembelewa na wageni wengi.

"Kwa hapa kwetu na sisi tutakaa na wenzetu kutatua changamoto hizi. Hapa tutajenga Maktaba ambapo watu watakuja kusoma vitabu vya Mwasisi wetu na kuona mambo aliyokuwa akifanya. Lakini pia tutaonana na Viongozi wa Halmashauri ya Kinondoni kuona namna ya kupaboresha mahala hapa ikiwemo miundombinu ya Barabara ya kuingia na kutoka eneo hili" alisema Dk. Kigwangalla.

Alisema maboresho mengine makubwa yatakayofanywa katika nyumba hiyo ni pamoja na kutengeneza choo, kupaka rangi na kufanya maboresho ya vionyeshwa vya kumbukumbu nzima ya Baba wa Taifa vilivyopo ndani ya nyumba hiyo ikiwemo kukuza picha na kuzijengea fremu za kisasa.

"Kiuhalisia hapa ni hazina kubwa sana ya kumbukumbu ya Taifa letu hasa katika harakati za kupigania Uhuru ambazo zilianzia hapa katika nyumba hii. Tutaiboresha zaidi kwa kuweka studio maalumu, tutaboresha CD zote za Baba wa Taifa na zitakuwa zikioneshwa humo ikiwemo zile za Hotuba zake," alisema Dk. Kigwangalla.

Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu wa Makumbusho hiyo, Neema Mbwana alisema changamoto zilizopo ni uchakavu wa nyumba hiyo na vioneshwa vilivyopo ambapo ameiomba Serikali kuboresha madhari ya nyumba hiyo na vioneshwa vyake ikiwemo kuzalisha nakala za kutosha za vitabu ambavyo ni mali ya baba wa taifa kutokana na kukabiliwa na uchakavu mkubwa.

Mbali na kutembelea Makumbusho hiyo, Dk. Kigwangalla pia alitembelea eneo la Mwenge wanapochonga na kuuza vinyago vya Makonde, na eneo la Oysterbay Morogoro Store wanapochora na kuuza picha za Sanaa ya Tingatinga.

"Tingatinga ni michoro ya miigizo isiyo halisi ya vitu mbali mbali inayochorwa kwa rangi 6 (mara nyingi). Mtu wa kwanza kuchora picha hizi ni marehemu Edward Saidi Tingatinga aliyevumbua uchoraji huu mwaka 1968 na kufanya kazi hiyo mpaka 1972 alipofariki.

"Sanamu za Makonde na picha za Tingatinga ni utambulisho mkubwa wa Sanaa ya Mwafrika nje ya bara letu na huvutia watalii wengi. Katika mikakati tuliyonayo ya kuongeza faida zinazotokana na utalii kwa wananchi tunakusudia kuboresha biashara kama hizi," alisema Dk. Kigwangalla.

© 2018 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top