You Are Here: Home » Whats New » IDADI YA WATALII NCHINI YAZIDI KUONGEZEKA

IDADI YA WATALII NCHINI YAZIDI KUONGEZEKA

 

 

IDADI YA WATALII NCHINI YAZIDI KUONGEZEKA.

Idadi  ya watalii walioingia hapa nchini imeongezeka kutoka Milioni 1.2 Mwaka 2016 hadi kufikia  Milioni 1.3 mwaka 2017

Taarifa hiyo imetolewa leo mjini Dar-es-Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Jen.  Gaudence Millanzi wakati wa uzinduzi wa ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Watalii Walioondoka nchini mwaka 2017'.

Maj. Jen. Milanzi amesema taarifa ya utafiti huo inaonesha kuwa Tanzania inazidi kufanya vizuri katika sekta ya utalii huku idadi ya watalii ikiongezeka mwaka hadi mwaka.

Amesema, mapato  kutokana na sekta ya Utalii yameongezeka kutoka Dola za Kimarekani  bilioni 2.2 Mwaka 2016 hadi kufikia Dola bilioni 2.3  Mwaka 2017.

Amezitaja sababu zilizochangia  ongezeko la watalii hapa nchini kuwa ni ongezeko la kasi ya Bodi ya Utalii Tanzania(TTB)  katika kuvitangaza  vivutio vilivyopo nchini  zikiwemo mbuga za wanyama, fukwe, mlima Kilimanjaro na vinginevyo pamoja na ujenzi wa barabara katika hifadhi za Taifa.

Maj. Jen Millanzi amesema, matokeo ya utafiti yanaonyesha idadi kubwa ya watalii walikuja kutembelea mbuga za wanyama na fukwe.

Utafiti huo umefanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Benki Kuu Tanzania (BOT), Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS),  Idara ya Uhamiaji, Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Shirikisho la vyama vya Utalii Tanzania ( TCT),  na Shirikisho la wawekezaji katika Sekta ya Utalii Zanzibar ( ZATI)

Maj. Jen. Millanzi amesema,  takwinu za utafiti huo,  zimepatikana kutokana na utafiti iuliofanywa  katika njia kuu za watalii, ikiwemo viwanja vya ndege  vya kimataifa pamoja na maeneo ya njia za  kuingilia na kutokea watalii.

Utafiti huo umeonyesha kuwa idadi kubwa ya watalii wametokea nchi za Marekani, Uingereza, Italy na Kenya.

Naye,  Kaimu Mkurugenzi wa Utalii  Wizara ya Maliasili na Utalii Deograsius Mdamu amesema, kwa sasa Wizara ya Maliasili na Utalii imeanza kuwekeza nguvu katika utalii wa fukwe kwa vile ni aina ya utalii ambao unaonekana kupendwa na watalii  wengi wanaoingia nchini.

Ameongeza kuwa, Wizara ya Maliasili na Utalii inatarajia kushirikiana na  mamlaka mbalimbali  ikiwemo Mamlaka ya Uendelezaji Uchumi(EPZA) katika kuendeleza utalii wa fukwe.

Amesema, Wizara ya Maliasili na Utalii inazifanyia kazi changamoto mbalimbali ambazo baadhi ya watalii wamekutana nazo ili kuhakikisha idadi ya watalii inazidi kuongezeka na vivutio vilivyopo hapa nchini vinatangazwa kwa kasi zaidi katika  jumuia ya kimataifa.

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top