You Are Here: Home » Whats New » Nyalandu : Kwanini Sijasaini Tozo Mpya za Hoteli za Kitalii.

Nyalandu : Kwanini Sijasaini Tozo Mpya za Hoteli za Kitalii.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Lazaro Nyalandu, amesema kwamba hawezi kusaini tozo zilizoidhinishwa kutokana na kutoorodheshwa kwa hoteli 30 kati ya 57 ndani ya hifadhi za taifa, ukadiriaji usiozingatia haki wa ukokotoaji wa tozo ni mojawapo ya masuala ya msingi yaliyomfanya Mhe. Nyalandu kuchelewa kutoa tangazo katika Gazeti la Serikali.

‘’Siwezi kukurupuka kusaini tozo hizo kwa kuwa zinahusisha hoteli 27 tu jambo ambalo si sawa kwani zimeachwa hoteli kubwa jambo ambalo halikubaliki kwa maendeleo ya nchi’’ Mhe. Nyalandu alisema.
Mhe, Nyalandu alisema yeye hasitahili kulaumiwa kwa kuchelewa kusaini tozo hizo kwa sababu Mawaziri waliopita ndio waliostahili kutia saini ingawa nao walishindwa kufanya hivyo.

‘’ Mimi ni Waziri na nina uchungu wa nchi yangu iwapo tu ningekubali kusaini,  hoteli chache zingeweza kulipa tozo hiyo na nyingine tena kubwa kutolipa, huku ukadiriaji na ukokotoaji kutokuwa na usawa hata kwa hoteli zinazolingana hadhi’’ Mhe Nyalandu alisisitiza.
Alikiri kuwa Serikali imepoteza pesa nyingi sana lakini hata hivyo kuchelewa kusaini tozo hizo mpya kunatokana na kufuta misingi ya Utawala bora kwa kuwa kulikuwa na kesi mahakamani kuhusiana na suala hilo ambalo lilidumu kwa miaka minane.

‘’ Hata wao wasingeweza kupitisha tozo hiyo kwa sababu ya utawala bora kwani tozo iliyokuwepo kisheria ni namba 50 ya mwaka 2002, inayowataka wageni kulipa asilimia 10 ya tozo ‘’alisema.
Alisema Shirika la Hifadhi ya Taifa ( TANAPA),lilitaka kulipwa tozo kamili na kutangaza tozo mpya 2007, jambo lililosababishwa kuwepo kwa kesi hiyo.
Mhe.Nyalandu, alisisitiza kuwa asingeweza kutia saini ndani ya mwezi mmoja pasipo kushauriana, kuchunguza vema mkataba huo na wataalam kabla ya kufanya uamuzi sahihi kwa kuwa bila kufanya hivyo ni kuliweka taifa kwenye hatari ya kupata hasara kubwa kimapato.

Aidha , Mhe. Nyalandu, jana amepokea magari makubwa manne yakiwemo mabasi mawili aina ya Marcopollo na maroli makubwa mawili aina ya Scania kwa ajili ya Chuo cha Pasiansi kilichopo mkoani Mwanza kwa lengo la kuwasafirisha askari Wanyamapori wakiwa kwenye mafunzo kwa vitendo ikiwa ni mikakati ya kuwandaa wahitimu wenye weledi wa kulinda rasilimali zetu.
Aliongeza kuwa, Magari hayo manne yatasaidia Chuo cha Pasiansi kurahisisha katika utoaji wa mafunzo ya kisasa kwa kuimarisha miundo mbinu itakayowawezesha kusafiri kwa urahisi wakati mafunzo kwa vitendo katika mapori mbalimbali nchini.
Alisema kuwa Magari hayo manne aina ya Scania na Marcopolo yenye thamani ya shilingi bilioni moja ikiwa ni msaada kutoka kwa   Howard Buffet mdau wa Uhifadhi raia wa nchini Marekani.

 

© 2018 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top