You Are Here: Home » Whats New » NAIBU WAZIRI MHE.HASUNGA AWEKA MIKAKATI YA SERIKALI YA KUVITANGAZA VIVUTIO

NAIBU WAZIRI MHE.HASUNGA AWEKA MIKAKATI YA SERIKALI YA KUVITANGAZA VIVUTIO

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ametaja mikakati ambayo Serikali inatarajia kuitekeleza ili kuhakikisha vivutio vilivyopo katika mkoa wa Njombe vinaboreshwa na kutangazwa ili viweze kujulikana ndani na nje ya nchi ili watalii waweze kuvitembelea

Amebainisha mikakati hiyo jana kwenye ziara yake ya siku moja mkoani Njombe wakati alipotembelea kijiji cha Mlevela, kata ya Mdandu wilaya ya Wanging’ombe ambapo aliweza kutembelea baadhi ya vivutio vya utalii kama vile Boma la Wajerumani, Kanisa la Kilutheri la Lupembe lenye miaka 108, Msitu asili wa Nyumbanitu, mapango ya nyumbanitu yenye historia na maajabu lukuki kuhusiana na nchi hii.

Amesema mikoa ya Nyanda za juu Kusini imejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii lakini vivutio hivyo vimekuwa havijulikani kwa sababu havijatangazwa vya kutosha.

Akitaja miongoni mwa mikakati hiyo, Naibu Waziri Hasunga amesema Serikali inategemea kutuma wataalamu kwa ajili ya   kuandaa makala maalumu za vivutio hivyo hali itakayosaidia   kuvitangaza vivutio hivyo ikiwa pamoja na kuweka kumbukumbu.

Pia,  Amesema Serikali inatarajia kutuma jopo la Wataalamu wa tasnia ya utalii kwa ajili ya kutoa ushauri pamoja na kuzungumza naWazee wa Baraza la kabila la Wabena ili kuona namna bora kuvibainisha na kuviboresha vivutio vya utalii ili viweze kujulikana na kuanza kutangazwa

Aidha, Amesema Serikali inategemea kujenga kituo cha maelezo ya Utalii katika eneo la Nyumbanitu, ambapo kituo hicho kitakasaidia watalii   kuweza kupata taarifa za kutosha kuhusiana na Msitu asili wa Nyumbanitu pamoja na maajabu yake wakati watalii hao watakapotembelea eneo hilo.

Alifafanua kuwa, Kituo kicho kitatumiwa na watalii wa ndani na nje ya nchi kupata taarifa mahsusi kuhusu mila na desturi za kabila la Wabena pamoja na kuburudishwa na ngoma za kabila hilo.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amesema Serikali inatarajia kukarabati boma la Mjerumani lililojengwa mwaka 1902 Ili liendelee kuwepo kwa vile lina historia ndefu ya mkoa huo, Aidha, eneo hilo ndipo chimbuko la neno Njombe ambalo limetokana na miti uliopo katika boma hilo unaoitwa Mdzombe.

Kwa upande wake Chifu wa Kabila la Wabena, Mkongwa ametoa wito kwa jamii ipende utamaduni wake kwa vile hakuna nchi yeyote duniani iliyoendelea kwa kuiga utamaduni wa taifa jingine.

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top