You Are Here: Home » Whats New » NAIBU WAZIRI KANYASU AIAGIZA TAWA KUUNDA CHOMBO CHA NDANI CHA KUZUIA RUSHWA

NAIBU WAZIRI KANYASU AIAGIZA TAWA KUUNDA CHOMBO CHA NDANI CHA KUZUIA RUSHWA

Kutokana na tuhuma za rushwa kuwakabili baadhi ya Maafisa Wanyamapori, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ameiagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania( TAWA) kuunda chombo cha ndani cha kuzuia na kupambana na Rushwa.

 

Akizungumza na Maafisa Wanyamapori hao jijini Dodoma mwishoni mwa wiki hii, Naibu Waziri Kanyasu amesema Chombo hicho kitakuwa na wajibu wa kuchunguza mienendo ya rushwa kwa watumishi hao ikiwa pamoja na kuwakamata wale wote watakaojihusisha kuomba na kupokea rushwa kutoka kwa wananchi.

Mbali na jukumu hilo, Chombo hicho kitashughulikia masuala ya nidhamu pamoja matumizi mabaya ya madaraka kwa Watumishi wa TAWA.

Pia amesema chombo hicho kitakuwa na jukumu la kuchunguza vitendo vya rushwa kwa Maafisa hao kabla ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kutekeleza jukumu hilo ikiwa lengo ni kutaka kumaliza kabisa tatizo hilo.


” Ninataka kabla ya TAKUKURU kuingia kwa ajili ya kuchunguza vitendo vya rushwa, Chombo hiki kitakuwa tayari kimeshawabaini watumishi ambao wapo kwa ajili ya maslahi ya matumbo yao.Alisema Kanyasu

Akizungumzia namna Chombo hicho kitakavyofanya kazi, Amesema chombo hicho kitafanya kazi nchi nzima na kitakuwa kila kanda na kusisitiza kuwa hakitakuwa makao makuu pekee kama vilivyo vitengo vingine.

“Undeni hiki chombo haraka iwezekanavyo haiwezekani wote mnaonekana ni wala rushwa ilhali kuna watumishi wachache wanaoipaka matope Taasisi hii” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu ameiagiza TAWA ibadilishe fomu ambapo mifugo ikikamatwa ndani ya Hifadhi Mchungaji atatakiwa kujaza baadhi ya taarifa muhimu ikiwemo kukiri mifugo kukutwa ndani Hifadhi.

Amesema hatua hiyo inakuja baada ya kugundua mapungufu makubwa kwenye fomu wanazozitumia kwa sasa, Kanyasu amesema fomu hizo mpya ziongezewe kipengele cha muda ambao mifugo imekamatwa na wakati huo Askari Wanyamapori wanatakiwa kuipiga picha mifugo ikiwa vielelezo vya ushahidi vitakavyotumika mahakamani wakati wa kesi.

Naye, Naibu Kamishina wa TAWA, Mabula Misungwi amesema malalamiko mengi ya wananchi kuhusiana na Wahifadhi yanahusu rushwa, kuundwa kwa chombo hicho kitasaidia kupunguza tatizo la rushwa kwa kuwabaini wale wote wenye tabia hizo.

Ameongeza kuwa Chombo hicho kitasaidia kupunguza tatizo la kuwaona Watumishi wote TAWA ni wala rushwa jambo linalopunguza ari ya kazi kwa baadhi ya watumishi wanaofanya kazi kwa misingi ya kufuata kanuni na sheria za utumishi wa Umma

Abel Kazoka ambaye ni Afisa Wanyamapori amesema kuundwa kwa chombo hicho kitasaidia kuwabaini wala rushwa badala ya kuwaona watumishi wote wa Taasisi hiyo ni wala Rushwa.

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top