You Are Here: Home » Whats New » MIKOA YA NYANDA ZA JUU KUSINI YAPIGIWA CHAPUO UTALII

MIKOA YA NYANDA ZA JUU KUSINI YAPIGIWA CHAPUO UTALII

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constanine Kanyasu ametoa wito kwa wafanyabiashara za utalii nchini kuwekeza katika mikoa ya Nyanda za juu Kusini ambayo ina vivutio vingi vya utalii.

Pia, Amesema kuwa wizara yake itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wafanyabiashara hao kwa kupunguza masharti kwa kampuni binafsi za utalii hasa za wazawa ili kuongeza tija katika biashara ya utalii nchini.

Amebainishwa hayo wakati Naibu Waziri huyo akifungua Maonesho ya tatu ya Utalii ya Karibu Kusini yanayofanyika katika viwanja vya Kichangani mkoani Iringa yenye kauli mbiu isemayo’’ Karibu Kusini Ufurahie Utalii Wetu’’

Akitaja mikoa hiyo ya Nyanda ya juu kusini kuwa ni Iringa, Mbeya, Njombe, Songwe, Ruvuma, Rukwa na Katavi, Mhe. Kanyasu amesema kuwa mikoa hiyo imejaliwa kuwa na idadi kubwa ya vivutio vya kihistoria, kiutamaduni na kiikolojia vinavyofanya upekee wa mikoa hiyo katika sekta ya utalii hapa nchini na ulimwenguni.

Sambamba na hilo, Mhe. Kanyasu amewataka wafanyabishara hao waanze kuwekeza miundombinu ya utalii kama vile kujenga hoteli pamoja na kufungua kampuni za utalii katika ukanda huo badala ya kuendelea kuwekeza zaidi katika mikoa ya Kaskazini.

Katika hatua nyingine,Mhe,Kanyasu ameiagiza Mikoa yote nchini kutenga bajeti kwa ajili ya kuendeleza vivutio vya utalii ikiwa pamoja na kuvitunza kuvitangaza vivutio hivyo.

Aidha, Mhe, Kanyasu amewasihi Wakuu wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kushiriki kikamilifu katika maonesho hayo kwa pamoja na kuwa na vikao vya mara kwa mara na wadau wa utalii katika Mikoa hiyo ili kuimarisha maendeleo ya sekta ya utalii katika mikoa hiyo.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bw. Richard Kasesela amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa Bodi ya Taifa ya Utalii (TTB) imeitenga mikoa hiyo kwa vile katika maonesho ya Utalii ya Nje za nchi, TTB imekuwa haivitangazi vivutio vilivyoko Nyanda za Juu Kusini.

Kufuatia hali hiyo, Mkuu wa Mkoa huyo amemuomba Naibu Waziri Mhe. Kanyasu aiagize TTB itoe kipaumbele kwa kutangaza vivutio vya mikoa hiyo katika maonesho ya ndani na nje ya nchi ili vivutio wa mikoa hiyo viweze kujulikana kama vivutio vya mikoa ya kaskazini.

Maonesho ya Utalii ya Karibu Kusini yalizinduliwa mwaka 2016 yakiwa yamelenga kuchochea maendeleo ya utalii kwa Mikoa ya Kusini kwa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika mikoa hiyo.

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top