You Are Here: Home » Whats New » MHE.KANYASU AWATOA HOFU WATUMISHI JUU YA MASLAHI BAADA YA UJIO WA JESHI USU

MHE.KANYASU AWATOA HOFU WATUMISHI JUU YA MASLAHI BAADA YA UJIO WA JESHI USU

Naibu Waziri Wizara ya Maliasili na Utalii, Mhe.Constantine Kanyasu amewatoa hofu watumishi wa Taasisi zenye jukumu la kulinda na kuhifadhi Wanyamapori na Misitu nchini kuwa hakuna maslahi yao yatakayobadilika baada ya ujio wa Jeshi Usu

Naibu Waziri Kanyasu ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro ikiwa ni mara yake ya kwanza kukutana na watumishi hao tangu alipoteuliwa kushika wadhifa wa Naibu Waziri katika Wizara hiyo nyeti kwa uchumi wa nchi.

Amesema ziara yake imelenga kuzifahamu Taasisi anazoziongoza ili kujua namna zinavyotenda kazi na changamoto zinazowakabili ili kuzipatia ufumbuzi.

Akizungumza kuhusu utendaji wa Jeshi USU, Naibu Waziri Kanyasu amesema kufuatia mabadiliko ya mfumo wa utendaji kutoka katika mfumo wa kiraia na kuwa Jeshi USU kutakuwa na mabadiliko kiutendaji yatakayoendana na taratibu za Jeshi USU lakini utakaoheshimu na kulinda maslahi ya watumishi. 

Naibu Waziri huyo ameeleza kuwa, uanzishwaji wa Jeshi hilo haukusudii kubadili maslahi ya watumishi hao na endapo maslahi hayo yatabadilika basi yatakuwa na mabadiliko chanya kwao.

Naibu Waziri Kanyasu ameongeza kuwa Jeshi USU litaongeza nidhamu uwajibikaji na maadili kwa watumishi wa sekta ya Maliasili na Utalii ili waweze kusimamia ipasavyo uhifadhi endelevu wa maliasili na si vinginevyo.

Katika hatua nyingine,  Naibu Waziri Kanyasu ameiagiza Menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro ibuni vivutio vipya vya Utalii vitakavyosaidia kuongeza mapato kwa Serikali kwa kuzingatia majukumu makuu ya Taasisi.


Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro, Freddy Manongi amewahakikishia watumishi hao kuwa maslahi yao hayatabadilika na ikiwezekana yataongezwa kwa sababu uwajibikaji utaongezeka baada ya ujio wa Jeshi Usu

Ameongeza kuwa mfumo wa Jeshi Usu haumaanishi kuwa Watumishi hawapaswi kupewa maslahi yao na badala yake yanahitaji kuboreshwa zaidi ili waweze kuwa na ari ya kufanya kazi katika kulinda Wanyamapori na Misitu nchini.

” Kati ya masuala ambayo nayapigania yasiweze kubadilika baada ya ujio wa Jeshi Usu ni maslahi yenu” amesema Dkt. Manongi.

Jeshi USU lilizinduziwa rasmi tarehe 17 Novemba mwaka huu na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan katika Uwanja wa Fort Ikoma wilayani Serengeti mkoa wa Mara.

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top