You Are Here: Home » Whats New » MAKAMU WA RAIS, MHE. SAMIA SULUHU HASSAN AWAONYA WAVAMIZI WA HIFADHI NCHINI

MAKAMU WA RAIS, MHE. SAMIA SULUHU HASSAN AWAONYA WAVAMIZI WA HIFADHI NCHINI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa onyo kwa wananchi wenye tabia ya kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya Hifadhi kuwa, waache mara moja na wale watakaoendelea wasije kuilaumu serikali kwa hatua zitakazochukuliwa dhidi yao.

Ameyasema hayo leo wakati akizindua rasmi Jeshi Usu ambalo limepewa jukumu la kulinda maliasili za nchi ikiwemo wanyama pori na misitu.

Katika uzinduzi huo umehusisha taasisi tatu za Wizara ikiwemo   Hifadhi za Taifa (TANAPA) Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyama pori Tanzania (TAWA) pamoja na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, ametoa wito kwa wananchi kuacha mara moja vitendo vya kuvamia hifadhi na kufanya ujangili, kuwa kwa sasa kipyenga kimepigwa, watakaokaidi wasiilaumu Serikali kwa hatua zitakazochukuliwa dhidi yao.

Aidha, Mhe.Samia ametoa rai kwa wanachi wanaoishi kuzunguka hifadhi, kutoa ushirikiano kwa Jeshi Usu ili kuweza kulinda usalama wao pamoja na Watalii.

Aidha, Mhe. Samia amesema ujio wa Jeshi hilo utasaidia kupambana na majangili ambao wamekuwa wakitumia silaha za kivita pamoja na kuwatambua magaidi wanaokuja wakijifanya ni watalii.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Nape Nnauye (MB) amesema operesheni za Jeshi Usu zitaendeshwa kwa kuzingatia haki za kibinadamu ili Wananchi waweze kuona thamani ya uhifadhi.

Awali, Waziri wa Malisili na Utalii Mhe. Hamisi Kigwangalla amempongeza Mhe.Rais, John Pombe Magufuli kwa kuridhia uanzishwaji wa jeshi hilo huku akiwataka watanzania kuwa wazalendo na wenye uchungu na maliasili zilizopo nchini.

Ameongeza kuwa, Jeshi Usu litachangia kuongeza nidhamu pamoja na uwajibikaji kwa askari hao.

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top