You Are Here: Home » Whats New » Maadhimisho ya Siku ya Kutundika Mizinga ya Nyuki Kitaifa

Maadhimisho ya Siku ya Kutundika Mizinga ya Nyuki Kitaifa

Maadhimisho ya Siku ya Kutundika Mizinga ya Nyuki Kitaifa

Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania itaadhimisha siku ya kutundika Mizinga Kitaifa tarehe 25 Machi katika Msitu wa Hifadhi Mtunguru uliopo kijiji cha Bogolwa, Wilayani Handeni, Mkoani Tanga.

Mgeni Rasmi katika shughuli hiyo ni Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Magalula Said Magalula ambaye ataongoza zoezi la kutundika Mizinga na kuhutubia Wananchi. Aidha katika Maadhimisho hayo kutakuwa na maonesho ya shughuli za Ufugaji Nyuki na Mazao ya Nyuki kuanzia tarehe 23 – 25 Machi 2015. Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku hii mwaka huu itakuwa “ Fuga Nyuki kwa kipato, Lishe na Mazingira bora”
Kwa miaka mitatu sasa Wizara ya Maliasili na Utalii imekuwa ikiadhimisha siku ya kutundika mizinga nchini ambapo kila mwaka katika siku hiyo baadhi ya mikoa Tanzania bara hushiriki zoezi hilo.Pia maadhimisho haya yatafanyika katika ngazi ya kanda, Mikoa na wilaya kulingana na kalenda ya ufugaji nyuki katika eneo husika.

Kulingana na takwimu za Shirika la Chakula Duniani(FAO),Tanzania ni nchi ya 2 kwa ufugaji nyuki Afrika baada ya Ethiopia, na huzalisha tani 34,000 za asali ambayo ni sawa na asilimia 24.6 ya uwezo wake wa uzalishaji. Uwezo huu wa uzalishaji ungeweza kuongezeka endapo juhudi za makusudi zitaelekezwa katika zao hili na kutoa matokeo bora zaidi kwa sababu mazingira yanayofaa kwa ufugaji nyuki nchini ni makubwa.
Katika juhudi za kuhamasisha ufugaji nyuki kwa kipindi cha miaka 3 (2010/11- 2012/13, jumla ya Manzuki 36 zenye mizinga 4,184 zimeanzishwa nchini katika Kanda 7 za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania.  Katika kipindi hicho kiasi cha tani 1,194 za asali zenye thamani ya shilingi 9,856,968,799 na tani 644.586 za nta zenye thamani ya shilingi 2,672,105,849 zilisafirishwa nje ya nchi. Aidha, jumla ya vikundi 921vyenye wafugaji nyuki 7,320 kutoka wilaya 30 za mradi wa kuboresha ufugaji nyuki (BIP) vimenufaika na mafunzo ya ufugaji bora wa nyuki.

Sera ya Taifa ya Ufugaji nyuki ya Mwaka 1998 inahimiza uanzishwaji wa hifadhi za nyuki za Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na watu binafsi ili kulinda makundi ya nyuki pamoja na malisho yao. Jumla ya Hekta 69,613 zimehifadhiwa ambapo hekta 37,166 ni za Serikali kuu na hekta 32,447 ni hifadhi ya Vijiji.
Sekta ya ufugaji nyuki ina mchango mkubwa katika maisha ya mwanadamu kwa kumpatia chakula, ajira na kipato. Wananchi hunufaika kutokana na mauzo ya asali, nta na mazao mengine ya nyuki, utengenezaji wa vifaa vya ufugaji nyuki, na huduma ya uchavushaji. Aidha sekta ya ufugaji nyuki hapa nchini uajiri takribani watu milioni nne. Ukilinganisha na shughuli nyingine uanzishwaji wa ufugaji nyuki hauhitaji mtaji mkubwa wala uangalizi wa kila siku wa Mizinga. Aidha, hauhitaji ardhi kubwa na yenye rutuba ili kufuga nyuki hivyo kulifanya zao hili kuwa chaguo la watanzania.

Ufugaji nyuki ni muhimu katika shughuli za kilimo , uhifadhi wa mazingira na mifumo ya ikolojia kutokana na huduma ya uchavushaji wa mimea ambayo ambayo huongeza ubora na wengi wa mazao.
Wizara inatumia siku hiyo kuhamasisha ufugaji nyuki nchini ambao ni muhimu katika kukuza uchumi wa Taifa, kuongeza kipato cha familia, lishe na kuhifadhi Mazingira. Mikoa na wilaya inaombwa kutunga mkono katika kuadhimisha siku hii katika maeneo yao kulingani na kalenda ya ufugaji nyuki katika eneo hilo.
Wananchi wote Mnakaribishwa.

Imetolewa na
Katibu Mkuu
Wizara ya Maliasili na Utalii

© 2018 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top