You Are Here: Home » Whats New » KATIBU MKUU, PROF.MKENDA ATOA WITO KWA WANANCHI KUTEMBELEA KITUO CHA MALIKALE CHA KUNDUCHI

KATIBU MKUU, PROF.MKENDA ATOA WITO KWA WANANCHI KUTEMBELEA KITUO CHA MALIKALE CHA KUNDUCHI

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Adolph Mkenda ametoa wito kwa wananchi kutembelea kituo cha Malikale cha kunduchi kwa kujifunza historia na kupumzika.

 


Amesema, kituo hiki kipo jijini Dar-es-Salaam kandoni mwa bahari ambapo kuna upepo mwanana, fursa ya kujifunza historia , michezo ya bahari na pia ni eneo zuri la kupumzikia.

Akielezea kuhusu umuhimu wa kituo hiki Prof. Mkenda amesema, kihistoria kina magofu ya makaburi ya Masultani zaidi ya watano na watu mbalimbali. Aidha kuna mabaki ya akiolojia kutoka karne ya 8 hadi ya 18.

Profesa Mkenda ameongeza kuwa, katika magofu hayo, kuna maandishi ya kiarabu yenye kusomeka juu ya historia ya masultani hao.

Profesa Mkenda pia ameelezea juu ya uzuri wa eneo hilo ikiwemo uoto wa asili, bustani ya miti inayoendana na historia ya makaburi pamoja na uwepo wa wanyama wadogowadogo kama Nyani na digidigi.

Akifafanua zaidi kuhusu historia ya makaburi hayo ya karne ya 17 na 18,  mkuu wa kituo hicho Mhifadhi Mkuu wa Mambo ya Kale,  Reinfrida Kapela , amesema katika kituo hicho kuna kaburi la Sultani Mwenye Matumaini Al - Barawi la karne ya 18,  kaburi la Mohamed Mwenye Matumaini Al - Barawi la larne ya 17 na Sultani Haji - Ahmed Al Barawi la Karne ya 18.

Mkuu huyo wa kituo ameyataja makaburi mengine yaliyopo kuwa ni ya Sultani Haji - Abubakar Al- Hatim la karne ya 18 na Sultani Mohamed Al- Barawi ( mtoto wa Mwenye Matumaini)

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top