You Are Here: Home » Whats New » KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII YAUNGA MKONO WANANCHI KUONDOLEWA HIFADHINI

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII YAUNGA MKONO WANANCHI KUONDOLEWA HIFADHINI

Na Hamza Temba - Bagamoyo, Pwani - Septemba 3, 2017

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii imeunga mkono uamuzi uliofikiwa na kamati maalum iliyoundwa na Serikali ya Wilaya ya Bagamoyo kwa ajili ya kutafuta suluhu ya kumaliza mgogoro wa ardhi baina ya Hifadhi ya Taifa ya Saadan na wananchi wa kitongoji cha Uvinje walioanzisha makazi ya kudumu ndani ya hifadhi ya Taifa ya Saadan kinyume cha sheria.

Kamati hiyo iliyoundwa na wajumbe watatu ambao ni Serikali ya Wilaya ya Bagamoyo, Uongozi wa Kitongoji cha Uvinje na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania(TANAPA) kupitia Hifadhi ya Taifa ya Saadan ilifikia maazimio kuwa wananchi wa kitongoji hicho walioanzisha makazi ndani hifadhi hiyo waondolewe kwa utaratibu wa kulipwa fidia ili kumaliza mgogoro huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Wilayani Bagamoyo, Mwenyekii wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhandisi Atashasta Ndetiye alisema baada ya kutembelea eneo hilo wamejiridhisha kuwa Kitongoji hicho cha Uvinje kimeanzishwa ndani ya eneo la hifadhi ambapo ni kinyume cha sheria.

"Kiuhalisia tumeona kuna kitongoji ndani ya hifadhi ya Taifa ya Saadan, tumewasikiliza wananchi, tumesikiliza upande wa Serikali, kwa mujibu wa taratibu na sheria wale wananchi wanapaswa watoe ushirikiano, tunaamini kuna taratibu za Kiserikali zinafanywa kuhakikisha wale wananchi wanalipwa ili waondoke kwa usalama" alisema Ndetiye.

Aliongeza, "tumeona jinsi ambavyo baadhi ya wananchi hawako tayari kulipwa, lakini nadhani wakieleweshwa vizuri wataelewa kuwa ile ni hifadhi ya Taifa, na kama ni hifadhi ya Taifa basi inahusu maslahi ya Taifa, hivyo kila mwananchi anatakiwa atoe ushirikiano ili angalao Serikali ifanye uwekezaji wa kueleweka"

Ndetiye alisema kamati hiyo imeshaweka maazimio kwa ajili ya kushauri Bunge ili liazimie ni nini kifanywe na Serikali kumaliza mgogoro huo. Alisema, "Kwa udharura wake na kutokana na maelezo ya mkuu wa Wilaya, kwa ujumla kamati inakubaliana nayo kwasababu ameeleza vitu ambavyo tumeona vina tija zaidi kwa watanzania na tunaenda kulishauri Bunge na Serikali haraka iwezekanavyo ili hatua ziweze kuchukuliwa kumaliza mgogoro huo".

Awali akielezea kuhusu mgogoro huo Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Hemed Mwanga alisema baada ya maazimio ya kamati iliyoundwa na Serikali ya wilaya kumaliza mgogoro huo baadhi ya wananchi walikubali maazimio yaliyowekwa ya kulipwa fidia huku wengine wakikaidi kuondoka akiwemo muwekezaji aliyeshikilia sehemu ya eneo hilo kwa zaidi ya miaka tisa bila kuwekeza mradi uliokusudiwa ambapo wamepewa kipindi cha mwezi mmoja waondoke kwa hiari kabla ya nguvu kutumika kuwaondoa.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Uvinje, Hussein Akida alisema kitongoji hicho kilianzishwa ndani ya kijiji cha Saadan katika Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani zaidi ya miaka 100 iliyopita huku kikiwa na ukubwa hekta 3,000 na mpaka sasa Kitongoji hicho kina wakazi wasiopungua 72. Aliiomba Serikali kutambua mipaka ya kitongoji hicho pamoja na kuwasogezea wananchi huduma za kijamii.

Baadhi ya wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii walitilia mashaka uwiano wa kimahesabu wa taarifa hiyo na uhalisia ambapo walihoji iweje kitongoji chenye miaka mingi kiasi hicho kiwe bado hakijapewa hati ya kuwa kijiji kamili pamoja na idadi ndogo ya wananchi wasiongezeka ndani ya muda mrefu wa miaka zaidi ya 100 toka kuanzishwa kwa Kitongoji hicho.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani alisema, mgogoro huo uko wazi na unapaswa kumalizika mara moja kwa kuwa Serikali ya Wilaya kupitia kamati iliyoundwa imeshafikia maazimio ya kuwaondoa wananchi walioanzisha makazi ndani ya eneo la hifadhi kinyume cha Sheria. Alitoa wito kwa wananchi kutii sheria za hifadhi na kuheshimu mipaka iliyowekwa kuepusha migogoro isiyo ya lazima baina ya Serikali na wananchi.

KWA PICHA KUHUSU ZIARA HIYO TEMBELEA BLOG YA WIZARA__________www.wizarayamaliasilinautalii.blogspot.com

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top