You Are Here: Home » Whats New » Bi. Flaviana Matata Ateuliwa Kuwa Balozi wa Kutangaza Utalii wa Tanzania Nje ya Nchi.

Bi. Flaviana Matata Ateuliwa Kuwa Balozi wa Kutangaza Utalii wa Tanzania Nje ya Nchi.

Bi. Flaviana Matata Ateuliwa Kuwa Balozi  wa Kutangaza Utalii wa Tanzania Nje ya Nchi.Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Adelhelm Meru akiwa na Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Taifa ya Utalii, Devota Mdachi akizungumza na Waandishi wa habari jana (hawapo pichani) mara baada ya kutangaza kumteua Balozi wa kutangaza vivutio vya Utalii vya Tanzania nchini Marekani, Bi. Flaviana Matata ( wa kwanza kulia) ambaye ni Mwanamitindo Maarufu anayefanya kazi zake za Mitindo katika Jiji la New York.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Adelhelm Meru na Waziri mwenye dhamana wamemteua Bi. Flaviana Matata ambaye ni mwanamitindo mzawa anayefanya kazi zake nchini Marekani kuwa Balozi wa kutangaza vivutio vya Utalii wa Tanzania nchini Marekani.
Akizungumza kwenye hafla fupi ya kumtangaza Balozi huyo iliyofanyika jana Makao makuu ya Wizara, Mpingo House , Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Meru alisema Wizara imejiridhisha vya kutosha kumteua Bi. Flaviana Matata kuwa Balozi wa kutangaza Utalii wa Tanzania katika jiji la New York kutokana na jitihada zake binafsi kabla ya kuteuliwa alikuwa mstari wa mbele kutangaza vivutio vya Utalii vilivyoko Tanzania katika shuguli zake za mitindo.

Kuchaguliwa kwa Flaviana Matata kuwa Balozi kumekuja siku chache baada ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, Jakaya Mrisho Kikwete kuzindua kampeni maalum ya kutangaza Utalii katika Nyanja za Kimataifa kupitia tangazo lisemalo ‘’ Tanzania ni roho ya Afrika. ( Tanzania is the soul of Africa)  Uzinduzi huo ulikuwa ni wakihistoria ulihudhuriwa na Mabalozi na wa Wakilishi kutoka Taasisi mbalimbali pamoja na wadau wa Uhifadhi nchini.
Dkt. Meru alisisitiza kuwa kupitia tangazo hilo Tanzania itaweza kupata watalii wengi kutoka nchi mbalimbali duniani , pia itaweza kuongeza pato la Taifa na wananchi wengi zaidi wataweza kupata ajira .
Aliongeza kuwa Utalii unachangia asilimia 18 katika pato la Taifa,  Kwa miaka miwili Utalii umeiingizia Tanzania kiasi cha shilingi billioni mbili.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Taifa ya Utalii Bi, Devotha Mdachi   amesema ana imani kubwa na Balozi Bi. Flaviana Matata kuwa atatangaza vizuri vivutio vya Utalii vilivyoko Tanzania huko Marekani.
Aliongeza kuwa kupitia umaarufu wake ataweza kuwavutiwa Watalii wengi zaidi kuja nchini kutembelea hifadhi za mbuga za wanyama pamoja na vivutio mbalimbali.
Naye , Flaviana Matata ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kumteua kuwa Balozi wa kutangaza vivutio vya Utalii vya Tanzania nchini Marekani ‘’ Kiukweli nimefurahi sana na pia napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Waziri Lazaro Nyalandu, Katibu Mkuu Dkt. Adelhelm Meru na Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Taifa ya Utalii Bi, Devotha Mdachi, kwa kuona umuhimu wangu na kunifanya kuwa Balozi. “ Flaviana Matata alisema

Alisema anajiskia fahari kuwa Balozi kwani amekuwa akitangaza Utalii wa Tanzania katika shughuli zake za mitindo na   mara nyingi amekuwa anakuja na rafiki zake kutoka Marekani kuja kutembelea mbuga zetu kwa mfano mara ya mwisho walikuja mwezi uliopita wakatembelea Ngororo wengine Mikumi,

Aliongeza kuwa nafasi aliyoipata atahakikisha anaongeza juhudi kwa kuleta ongezeko kubwa la watalii kufahamu Utajiri uliopo nchini hasa katika sekta ya Utalii nchini ili kukuza pato la Taifa

© 2019 - Ministry of Natural Resources and Tourism Tanzania

Scroll To Top